Mwenyekiti Chadema mbaroni uchaguzi mitaa

JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limemkamata Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kilimanjaro, Gervas Eliewaha Mgonja (42).

Mgonja anatuhumiwa kutoa kauli za kuhamasisha wananchi kuvamia makazi ya wasimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa mkoani humo.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa ilisema alikamatwa baada ya kuonekana video mjongeo iliyosambaa katika mitandao ya kijamii akiwa anahamasiha wananchi kufanya uhalifu huo siku ya uchanguzi.

Advertisement

Maigwa alisema, “Maneno hayo ya kuhamasisha vurugu aliyatamka hadharani Novemba 24, 2024 na baada ya kutamka waliyasambaza katika mitandao ya kijamili”.

Alisema mtuhumiwa alichukuliwa maelezo ili hatua nyingine za kisheria zifuate.

Jeshi la Polisi la mkoa huo lilitoa onyo kwa yeyote atakayethubutu kufanya vitendo vyenye viashiria vya uvunjifu wa amani kabla, wakati na baada uchaguzi kwamba hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.