Mwenyekiti CHAKUHAWATA azikwa Kigoma

KIGOMA; Mamia ya wananchi wakiongozwa na viongozi wa Chama Cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu (CHAKUHAWATA) mkoani Kigoma na mikoa mbalimbali ya Tanzania katika mazishi ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho Steven Sabibi (70) yaliyofanyika Kijiji cha Kalinzi, Wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma.

Sabibi ambaye alikuwa mwanzilishi wa CHAKUWAHATA, akiwa mwenyekiti wa chama hicho tangu kilipopata usajili mwaka 2015 hadi umauti ulipomkuta,  Jumanne wiki hii Hospitali ya mkoa Kigoma, Maweni alipokuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumza katika misa ya mazishi kwenye Kanisa Anglikana Kijiji cha Kalinzi, Makamu   Mwenyekiti wa chama hicho, Ashery Ntayomba, amesema marehemu Sabibi atakumbukwa kwa misimamo yake ya kupinga rushwa na kutetea haki za wafanyakazi, zilizosababisha kuanzishwa kwa CHAKUHAWATA, baada ya baadhi ya walimu kujiengua na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT).

Akifafanua zaidi amesema marehemu alipata mafunzo ya sanaa za maonesho,  michezo, muziki na elimu ya usimamizi wa uanzishaji wa vyama vya wafanyakazi  katika nchi za Urusi, Jamhuri ya Check, Uswis na  Slovania na kwamba atakumbukwa kwa kazi kubwa ya kufundisha muziki na michezo aliyofanya katika shule mbalimbali mkoani Kigoma.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa CHAKUHAWATA, Twalib  Nyamkunga akizungumza katika misa ya mazishi alisema kuwa marehemu alitumia nguvu na juhudi zake kuhakikisha chama hicho kunakuwa na mafanikio, hivyo kuwezesha CHAKUHAWATA kwa sasa kuwa na wanachama 31,000 mikoa yote ya Tanzania kutoka waanzishi 180 waliokuwepo mwaka 2015.

 

Habari Zifananazo

Back to top button