Mwigulu awapa onyo watumishi wanaowanyima haki wananchi

IRINGA: WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Serikali haitasita kuwaondoa kazini watumishi wa umma watakaobainika kuwanyima wananchi haki zao au kuwazungusha bila sababu wanapohitaji huduma katika ofisi za umma.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Jimbo la Ismani uliofanyika katika Kata ya Kihologota mkoani Iringa, Dk Nchemba alionesha kutoridhishwa na tabia ya baadhi ya watumishi wanaowapa wananchi usumbufu usio wa lazima badala ya kutatua changamoto zao kwa wakati.

Amesema utumishi wa umma ni dhamana ya kuwahudumia wananchi na si fursa ya kuonesha mamlaka, hivyo Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na maadili ya kazi.

“Wananchi wanapofika katika ofisi za Serikali wanahitaji huduma, si kuzungushwa. Mtu anayenyimwa haki yake au kucheleweshwa bila sababu anakuwa anazuiwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Serikali haitavumilia hali hiyo,” alisema Dk Nchemba.

Alisisitiza kuwa mishahara ya watumishi wa umma inatokana na kodi zinazolipwa na wananchi, hivyo kila mtumishi anawajibika kutoa huduma kwa weledi, heshima na uadilifu.

Waziri Mkuu alisema baadhi ya wananchi hujinyima mahitaji muhimu ili kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi, jambo ambalo linaipa Serikali uwezo wa kujenga shule, vituo vya afya, barabara na kugharamia mishahara ya watumishi wa umma.

Kutokana na hali hiyo, alisema hakuna sababu kwa mtumishi kumdharau mwananchi au kumpotezea muda kwa urasimu usio na tija.

Aidha, alikemea tabia ya baadhi ya watumishi kutumia muda mwingi kwenye simu za mkononi au mazungumzo yasiyo ya kazi wakati wananchi wakisubiri huduma, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinadhoofisha taswira ya Serikali na kuondoa imani ya wananchi kwa taasisi za umma.

Dk Nchemba aliwataka wananchi kutokuwa waoga wanapofika katika ofisi za Serikali kutafuta huduma, akieleza kuwa wana haki ya kuhudumiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Pia alipendekeza watumishi wote wa umma kuvaa vitambulisho vyenye majina yao kamili ili kurahisisha uwajibikaji na kuwabaini wale watakaokiuka maadili ya kazi.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu aliwahakikishia wananchi wa Ismani kuwa Serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto zao pamoja na kutekeleza ahadi zote za maendeleo zilizotolewa kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Ismani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda, aliiomba Serikali kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya katika kata za Nyang’oro na Izazi, upatikanaji wa mashine ya X-Ray katika Kituo cha Afya cha Kihologota, ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kiume na kuharakisha mchakato wa kuanzishwa kwa Halmashauri ya Ismani.

Mtatifikolo alisema utekelezaji wa miradi hiyo utasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Ismani, huku akimshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo zinazowanufaisha wananchi wa jimbo hilo.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button