Mwinjuma amsifu Kiruswa kuendeleza riadha Longido

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Hamis Mwinjuma amempongeza Mbunge wa Jimbo la Longido mkoani Arusha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa kwa kutekeleza kwa vitendo Sera ya michezo kwa kuendeleza mchezo wa riadha jimboni hapo.

Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Michezo (BMT), Neema Msita amezungumza hayo kwa niaba ya Naibu Waziri huyo mara baada ya kumalizika kwa mbio za riadha za ‘Kiruswa Funrun Marathon’ zilizofanyika uwanja wa Longido na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 800.

Neema alisema Kiruswa anapaswa kupongezwa katika kutekeleza kwa vitendo Sera ya kukuza mchezo wa riadha na kuamua kujitoa na kuwapa nafasi washindi wanne kwenda kusomea vyuo vya michezo nchini Kenya ili kuumudu mchezo huo na kuitangaza nchi kimataifa.

Alisema mchezo wa riadha ni mchezo muhimu na ni ajira kubwa kwa kuliona hilo, Kiruswa ametoa motisha kwa washindi kwenda katika vyuo vya riadha nchini Kenya kujifunza zaidi mchezo huo ili kuwa wawakilishi wazuri katika michezo ya kimataifa.

“Serikali inahitaji kwa kiasi kikubwa watu wa aina ya Kiruswa kwani ni kiongozi mwenye moyo wa kujitoa katika kutekeleza sera ya michezo nchini hivyo serikali tunampa pongezi katika kufanikisha hilo,”alisema Neema.

Naye Mbunge Kiruswa alisema dhumuni la yeye kuamua kuwapeleka washindi wanne nchini Kenya kusomea zaidi mchezo wa riadha ni kwa sababu nchi ya Kenya inafanya vizuri katika mchezo huo na sio aibu kwa sisi watanzania kwenda kuongeza ujuzi kwao.

Alisema Kiruswa Funrun Marathon ambayo hufanyika kila mwaka katika kipindi cha mwezi mei mbali ya kujenga afya na kutokomeza magonjwa nyemelezi pia mchezo huo umekuwa ikiwakusanya vijana wengi katika jimbo la Longido na nje na kuratibiwa na uongozi wa riadha Mkoa ili kupata washindi vijana na wenye sifa katika mchezo huo.

Naye Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma aliwataka wana Longido kutomtupa Kiruswa kwani Kiruswa ni lulu adimu katika jamii ya wafugaji wa kimasai na kusema kuwa ni mtu mpole na msikivu lakini ni mchapakazi aliyeaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Msukuma alisema amekuja mara zaidi ya tatu katika jimbo la Longido na mara ya kwanza alipokuja kumnadi kwa mara ya kwanza mwaka 2018 na baadae kuaminiwa na Rais kwa kuwa amesoma vizuri na mwenye uelewa wa hali ya juu hivyo wanapaswa kumfikiria kuongoza tena jimbo hilo wakati ukifika kwa kuwa serikali inahitaji sana wasomi wa aina ya Kiruswa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salumu Kally amesema Longido pamoja na kuwa na jiografia ngumu ila wananchi wake wanapenda michezo na ndio maana Kiruswa amekuwa akifanya mara kwa mara mashidano ya riadha na soka lengo ni kutaka kuwapa ajira vijana.

Wakati huohuo katika mbio za km 21 wanaume ,Poul Matiko ameshika nafasi ya kwanza na kufanikiwa kujinyakuliwa zawadi ya Sh 500,000,Livingston Lameck alishika nafasi ya pili na kupata Sh 300,000,mshindi wa pili Ezekiel Mollel alipata Sh 250,000 na upande wa wanawake mshindi wa kwanza kwa mbio hizo alikuwa Paticia Mabena alipata zawadi ya Sh 500,000 na mshindi wa pili Stella Makula alipata Sh 300,000.

Mbio za km 10 wanaume mshindi wa kwanza Lowassa Sabore alipata Sh 250,000,nafasi ya pili ilichukuliwa na Baltazal Baltazal alipata Sh 200,000 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Mbaraka Kanyongo aliyeambula Sh 150,000 na upande wa wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Sarafina Abel alipata Sh 250,000 na nafasi ya pili alikwenda kwa yunes Yohana alipata Sh 200,000 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Dorin Kamsika aliyepata Sh 150,000.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button