RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi ametoa rai ya kuyafanya Mashindano ya Kuhifadhi Quraan Afrika kuwa ya ngazi ya kidunia.
Dk Mwinyi ametoa Rai hiyo alipozungumza katika Mashindano ya Kuhifadhi Quraan Afrika yaliyofanyika Uwanja wa New Amani Complex, Wilaya Mjini.
Ameeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika miaka miwili ya mashindano hayo Zanzibar yana kila sababu ya kuyapandisha ngazi na kuwa ya Kidunia.

Amesema Mashindano ya Kuhifadhi Quraan Afrika ni tukio liengine muhimu la kuutangaza utalii wa Zanzibar kimataifa kupitia matamasha na matukio ya aina hiyo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika na kutekeleza masuala ya kidini kwa pamoja.

Dk Mwinyi ameeleza kuwa umahiri wa kuhifadhi Quraan unaooneshwa na vijana ni urithi muhimu kwa vizazi vya sasa na baadae na kusifu juhudi za walimu wa madrasa na kuahidi Serikali kuunga mkono mashindano hayo.
Kwa upande mwingine, Rais Mwinyi amelipongeza Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuyaandaa mashindano hayo kwa mwaka wa pili kwa mafanikio pamoja na wadau wote waliochangia kufanikisha mashindano hayo.