Mwinyi apeleka neema kwa wakulima wa karafuu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Serikali itaendelea na sera ya utoaji wa asilimia 80 ya bei ya zao la karafuu kwa mkulima, ili kuinua kipato chao na kuchochea uzalishaji wa zao hilo.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo , tarehe 23 Oktoba 2025, katika hafla ya kukabidhi hati miliki za mashamba kwa wakulima wa karafuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Umoja ni Nguvu wa Baraza la Mji Mkoani, Pemba. Ameeleza kuwa Serikali bado inatambua umuhimu wa zao hilo kwa uchumi wa nchi na maisha ya wakulima, na itaendelea kuimarisha ongezeko la uzalishaji. SOMA: Wakulima wa karafuu kumiliki mashamba
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi amekabidhi boti ya wagonjwa (ambulance boat) kwa ajili ya wananchi wa visiwa vya Panza na Makoongwe, hatua itakayosaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma za matibabu katika maeneo hayo. Hafla hiyo imefanyika katika Bandari ya Mkoani. Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amekabidhi gari kwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kwa ajili ya kuimarisha ufuatijali wa mashamba ya karafuu.