Mwinyi: EU ina mchango mkubwa Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi amefahamisha kuwa Umoja wa Ulaya(EU) una mchango mkubwa na muhimu kwa maendeleo na sekta ya uwekezaji pamoja na ustawi wa maisha ya Wananchi.
Rais Dk Mwinyi amesema hayo alipofungua Kongamano la Biashara la Zanzibar na Umoja wa Ulaya, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Ameuhakikishia Umoja huo kuwa Serikali inachukua juhudi maalum kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji hapa nchini ili wawekezaji wanaokuja wawekeze katika mazingira bora na endelevu.
Halikadhalika, amesema Zanzibar itaendelea kushirikiana na EU katika nyanja mbalimbali za maendeleo kwani ni mshirika muhimu katika juhudi za kukuza uchumi.

Amebainisha kuwa uwekezaji wa Umoja wa Ulaya visiwani Zanzibar unachangia asilimia 31 ya miradi yote ya uwekezaji iliyosajiliwa unaofikia thamani ya Euro Bilioni 2.8 na kutoa fursa za ajira Elfu-19.
Rais Dk Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Ushirikiano Baina ya Umoja wa Ulaya na Mamlaka ya Uwekezaji ya Zanzibar (ZIPA) pamoja na kuzindua Ripoti ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya Zanzibar ya Mwaka 2023.



