Mwinyi: SMZ itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye Bima

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye soko la Bima ili kuongeza pato la taifa kupitia sekta hiyo.
Dk Mwinyi ameyasema hayo alipopokea taarifa ya Soko la Bima kwa Mwaka 2023 hafla iliofanyika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo kwa wananchi kutokana na mageuzi makubwa yanayoendelea kufanyika katika sekta zote za kiuchumi.
Amefahamisha kuwa ili mageuzi hayo yafanikiwe ni vema sekta ya Bima iendane na kasi ya Serikali zote mbili kwa kujikita kwenye ubunifu na matumizi ya teknolojia na watoa huduma za Bima na wadau wote wafanye kazi kwa weledi na ushirikiano.
Halikadhalika Dk Mwinyi amesisitiza kuongezwa jitihada zaidi katika matumizi ya TEHAMA,  ubunifu wa bidhaa za Bima na utoaji wa elimu ya Bima kwa wananchi.
Vilevile amebainisha kufanyika kwa utafiti wa aina ya vihatarishi vinavyotakiwa kupewa kinga kupitia Bima kwa mali za Serikali na Mamlaka ya Bima ipitie Sheria na Kanuni mbalimbali za Bima ili ziendane na mazingira ya sasa na ukuaji wa uchumi.
Kwa upande mwingine Dk Mwinyi amewasisitiza wananchi na wadau kuendelea kutumia huduma za Bima na mamlaka husika kufanya bidii ya kuhakikisha nchi inanufaika na huduma hizo.
Ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kwa kuanzisha ofisi ya TIRA kanda ya Unguja na ofisi ya Kanda ya Pemba na kusisitiza kutolewa elimu zaidi kwa wananchi ili wapate uelewa zaidi wa masuala ya Bima.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button