Mwisho malalamiko ya usaili TRA leo

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema leo ni mwisho wa kupokea malalamiko au ufafanuzi kuhusu matokeo ya usaili wa ajira katika taasisi hiyo.

Matokeo ya usaili huo yalitolewa Aprili 26, mwaka huu na TRA ilianza kupokea malalamiko au maombi ya ufafanuzi jana.

Hayo yalielezwa kupitia taarifa ya TRA kwa umma kuhusu uwasilishaji wa malalamiko hayo na kueleza kuwa hilo linafanyika kuhakikisha kila msailiwa anapata haki anayostahili.

TRA ilieleza malalamiko hayo yatatakiwa kuwasilishwa kwa njia ya barua kwa Kamishna Mkuu wa TRA kueleza sababu za malalamiko yao.

“TRA inapenda kuwafahamisha wasailiwa ambao wana malalamiko au ufafanuzi wowote kuhusiana na matokeo hayo kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya barua kwa Kamishna Mkuu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndani ya siku mbili kuanzia Aprili 28 hadi 29, 2025 wakieleza sababu za malalamiko yao,” ilieleza taarifa ya TRA.

Kwa wasailiwa waliopo Mkoa wa Dar es Salaam, TRA ilisema wanaweza kupeleka barua hizo kwenye ofisi ya TRA ya Kituo cha Huduma kwa Mlipa Kodi kilichopo Mtaa wa Samora wakati wa saa za kazi.

Taarifa ya TRA kwa umma ya Aprili 26, kuhusu matokeo ya usaili wa kuandika, iliwataarifu wasailiwa wote waliofanya usaili wa kuandika Machi 29 na 31, mwaka huu katika vituo tisa vilivyokuwa vimeandaliwa hapa nchini kuwa matokeo ya usaili huo yamekamilika na kuwa yanapatikana katika tovuti ya mamlaka.

Aprili 27, mwaka huu TRA pia iliwatarifu wasailiwa waliofaulu mtihani wa mchujo na kuchaguliwa kwamba usaili wa vitendo na mahojiano unatarajiwa kufanyika Mei 2, 2025 na hatimaye itawaajiri watakaofaulu usaili huo.

Aidha, TRA ilitangaza nafasi za kazi kuanzia Februari 6 hadi 10, 2025 na Machi 21,2025 ikatoa taarifa kwa umma kwamba baada ya kufunga mchakato wa kupokea maombi, jumla ya maombi 135,027 yalipokelewa.

Ilieleza kuwa kati ya hayo maombi 112,952 yalikidhi vigezo vya kuitwa kwenye usaili wa kuandika.

“Machi 23,2025 Mamlaka ilitoa fursa ya siku mbili (Machi 24 na 25, 2025) kwa waomba kazi ambao walidhani walistahili kuitwa kwenye usaili wa kuandika ila hawakuitwa na baada ya kutolewa kwa fursa hiyo jumla ya maombi 71 yalikidhi vigezo na hivyo kufanya jumla ya maombi 113,023 kukidhi vigezo vya kufanya usaili wa kuandika,” ilieleza taarifa ya TRA ya Aprili 2, 2025.

TRA ilisema wapo waombaji walioomba nafasi zaidi ya moja maombi 113,023 yaliyokidhi vigezo vya kufanya usaili wa kuandika yaliombwa na waomba kazi 86,314.

Kati yao, waombaji waliofanya usaili wa kuandika walikuwa 78,544 ambao ni sawa na asilimia 91 na waombaji 7,770 ambao ni sawa na asilimia tisa hawakushiriki kwenye usaili kutokana na sababu mbalimbali.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button