My Legacy yajitosa sekta ya elimu

DAR ES SALAAM: TAASISI isiyo ya Kiserikali ya My Legacy imejenga vyoo vitano vyenye matundu 20 katika shule za Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Februari 9,2024 Mratibu wa Programu kutoka My Legacy, Amina Ally amesema shule walizojenga vyoo ni nne za sekondari na moja ya msingi.

Amezitaja shule hizo kuwa ni Kisauke, Twiga, Maendeleo na Daniel Chongolo kwa shule za sekondari wakati  shule ya msingi iliyonufaika ni Mtakuja Beach.

Amesema, wameamua kujenga matundu ya vyoo katika shule hizo kutokana na Uhitaji wa vyoo kwa watoto wa kike ambao baadhi yao hulazimika kukatisha masomo siku za hedhi kutokana na kukosa sodo na sehemu ya kujihifadhi.

“Uhitaji bado ni mkubwa kwa watoto wa kike, tunajitaidi kadri tukavyoweza kufikia shule nyingi zaidi, tutaendelea kushirikiana na serikali na wadau kutatua changamoto za watoto wa kike ili waweze kusoma wakiwa huru, kwenye mazingira ya staha na kufurahia mazingira ya shule ya kujifunzia,”amesema.

Aidha, amesema pia taasisi hiyo ya My Legacy imetoa elimu ya ujuzi kwa wanafunzi kupitia klabu zao za shule, kuhakikisha jamii zinaishi maisha ya staha  na zinatokomeza umaskini.

Ujuzi wanaofundishwa ni kutengeneza batiki, sabuni, kupanda miti ya matunda, miti ya kivuli, bustani za mboga mboga na kutengeneza sodo.

Pia wanafundisha wanafunzi hao masuala ya uongozi, hedhi salama na usafi wa  hedhi

“Tumewafundisha kutengeneza sodo, hii inatatua changamoto za watoto wa kike ambao wazazi wanashindwa kumudu gharama na kujikuta siku za hedhi wanashindwa kwenda shule….; “Kwa hiyo unakuta wana ‘stock’ ambazo zinasaidia wale wenzao ambao hawana uwezo wa kununua, sodo hizi ni za kufua.

Aidha amesema pia wanafanya kazi na makundi mbali mbali ikiwa ni uwezeshaji wa wanawake, na vijana kiuchumi na uongozi shirikishi, utetezi wa haki za wanawake na watoto, masuala ya ukatili wa kijinsia na masuala ya uongozi.

Wakati huo huo Meshacky Daniel Afisa Mawasiliano My Legacy amewataka vijana ambao wapo vyuoni au wale ambao wamemaliza wajenge utamaduni wa kujitolea kwenye mashirika kwani inasaidia kuwapa ‘Networking’ na pia kujitolea ni njia ya kuitumikia jamii.

Cathereen Austine, Afisa Mradi wa My Legacy amesema  wanafunzi wengi wa vyuo wanakua na matumaini makubwa  yaani wakimaliza chuo waajiriwe kwenye taasisi kubwa, lakini sio fikra chanya zaidi, kujitolea ni mwanya mzuri wa kujitengenezea kukua kitaaluma lakini pia ni njia nzuri ya kutengeneza ‘connection’.

Amesema mwaka jana pekee ameweza kuwafikia mabinti 5,000 katika shule za wilaya tatu za Kawe, Kunduchi na Wazo kupitia program ya Wash ambayo waliwanoa kuhusu masuala ya hedhi salama, uongozi na kuwapatia ujuzi wa kutengeneza vitu mbali mbali.

Habari Zifananazo

Back to top button