‘Mzee Mkapa ni mfano wa kuigwa’

MTWARA; Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk Hussein Ali Mwinyi, ameeleza kuwa Hayati Mzee Benjamin Mkapa atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi cha sasa na kijacho kutokana na mchango wake mkubwa katika kujenga misingi ya maendeleo, utawala bora na ustawi wa Taifa.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Tanzania ilijenga nguzo muhimu za umoja wa kitaifa, Muungano, amani na mshikamano wa Watanzania, pamoja na nafasi ya Tanzania katika Bara la Afrika na ulimwenguni.

Rais Dk Mwinyi ameyasema hayo alipomwakilisha Rais wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, katika Ibada Maalum ya Kumbukumbu ya Miaka Mitano ya kifo cha hayati Benjamin William Mkapa, iliyofanyika leo Julai 23, 2025 Lupaso, Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amekumbusha kuwa hayati Mzee Mkapa alikuwa muumini wa ujamaa na uchumi wa soko unaoongozwa na sekta binafsi, lakini pia alihakikisha kuwa maendeleo yanawanufaisha wananchi wote bila ubaguzi.

Ameeleza kuwa hayati Mkapa ndiye aliyeanzisha Dira ya Maendeleo 2025, ambayo imekuwa chombo muhimu katika mageuzi ya maendeleo, na mafanikio yake yamekuwa msingi wa kuzinduliwa kwa Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Ametoa wito kwa viongozi wa dini, wanasiasa na wanahabari kuwa sehemu ya kulinda na kuendeleza tunu ya amani kama njia ya kumuenzi Mkapa.

Amesema kuwa Watanzania wanayo sababu ya kujivunia viongozi waliopo ambao wanaendeleza maono ya viongozi waasisi na kuipeleka Tanzania mbele katika nyanja zote za maendeleo.
Rais Dk Mwinyi alizuru kaburi la hayati Mkapa na kuweka shada la maua, akiongozana na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Filipe Nyusi, na kewe pamoja na Mjane wa hayati Mkapa, Mama Anna Mkapa. Hayati Mzee Mkapa alifariki dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020 akiwa na umri wa miaka 81, jijini Dar es Salaam.



