Mzunguko wa kwanza ulivyokula vichwa vya makocha
MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara umekamilika, baada ya kila timu kucheza michezo 15 wakati huo huo bado siku chache dirisha dogo kufungwa, ambalo lilifunguliwa Desemba 15, likitarajiwa kufungwa Jumatano ijayo Januari 15, 2025.
Kati ya timu 16 zinazoshiriki ligi hiyo, 12 zimeanza mzunguko wa pili kwa maana ya kucheza mchezo wa 16 isipokuwa Simba, Yanga, Tabora United na Kagera Sugar.
Katika muktadha wa mpira wa miguu, neno dirisha dogo hurejelea kipindi kifupi ambacho timu zinaruhusiwa kufanya mabadiliko ya wachezaji, yaani kuwasajili au kuwaachilia watoke.
Lengo ni kutumia nafasi hiyo kuimarisha vikosi vyao kwa kusajili wachezaji wapya, kuachana na wachezaji ambao hawana mchango wa kutosha au ambao wanataka kuondoka.
Lakini kwa upande wa makocha hali ni tofauti kwani wao hawana dirisha dogo wala kubwa, wakati wowote wanaweza kuajiriwa na kutimuliwa pindi tu klabu inapoona mambo yanakwenda mrama.
Timu zinatarajia mafanikio ya haraka, na ikitokea matokeo mabaya makocha huchukuliwa kama wahusika wakuu na kutwishwa mzigo huo wa lawama.
Ingawa sababu za ujumla za makocha kufutwa kazi ni pamoja na matokeo yasiyoridhisha kama vile kushindwa mara kwa mara, kutoendelea hatua za mbele kwenye mashindano na kushuka daraja, zikiwekwa kwenye kapu moja la mwenendo wa timu usioridhisha.
Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/2025, iliyoanza kutimua vumbi Agosti 16 mwaka jana imefikia nusu ya safari yake huku ikishuhudiwa makocha watano tu walioanza pamoja na timu zao wakisalia.
Makocha waliohimili mikiki mikiki ya ligi hiyo ni Fadlu Davids wa Simba, Mohamed Abdallah ‘Bares’ wa Mashujaa, Hamady Ally wa JKT Tanzania na Mecky Maxime wa Dodoma Jiji.
Mohamed Muya wa Fountain Gate alimaliza salama mzungo wa kwanza, lakini akakutana na mkono wa kwaheri kwenye mechi yake ya kwanza ya mzunguko wa pili, muda mfupi baada ya mechi yao dhidhi ya Yanga kumalizika na kupokea kipigo cha mabao 5-0.
Makocha walioishia njiani katika mzunguko wa kwanza ni pamoja na Youssouph Dabo wa Azam FC aliyetimuliwa Septemba 3, 2024 pamoja na benchi lake la ufundi ambalo lilikuwa na wasaidizi watano.
Dabo alihudumu kwenye kikosi hicho kwa mwaka mmoja na kuifanya Azam FC kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara 2023/2024 hadi kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika michezo ya awali ya Ligi ya Mabingwa hakuwa na mwanzo mzuri baada ya kutolewa na APR ya Rwanda, Agosti 18, mwaka jana. Alianza kwa ushindi wa bao 1-0 akiwa nyumbani Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.
Lakini kibao kiligeuka alipokwenda Kigali Rwanda na kufungwa kwa mabao 2-0 dhidi ya APR kwenye mchezo wa marudiano na kupoteza nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Hata hivyo mchezo wa kwanza wa ligi kuu, Azam walianza kwa suluhu dhidi ya JKT Tanzania, Agosti 28 mwaka jana na huo ulikuwa mchezo wake wa mwisho akiwa na Wanalambalamba.
Septemba 7, mwaka jana Rachid Taoussi raia wa Morocco alirithi mikoba ya Dabo.
Pamba Jiji waliopanda daraja msimu huu wakianza kwa kusuasua kwa kucheza michezo 10 ya awali bila ushindi hawakusita kuachana na Goran Kopunovic Octoba 16, mwaka jana.
Taarifa ya Pamba iliyotolewa na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu Ezikiel Ntibikeha ilisema pamoja na kumfuta kazi Mserbia huyo pia, ilisitisha mikataba ya wasaidizi wake Salvatory Edward, Kocha wa magolikipa, Razack Siwa na kocha wa viungo Circus Kakooza.
Kwa wakati huo kikosi cha Pamba kiliachwa chini ya kocha wao, Mathias Wandiba aliyekuwa akifundisha timu ya vijana chini ya miaka 20 klabuni hapo.
Kocha mwingine aliyeachia ngazi kwenye mzunguko wa kwanza ni Fikiri Elias wa KenGold, yeye aliomba kupisha Septemba 16, 2024 mara baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa KMC FC akiwa ugenini.
Klabu hiyo iliridhia ombi lake la kuondoka, pamoja na kocha wake msaidizi Luhaga Makunja, waliondoka wakiwa wamecheza michezo mitatu ya ligi kuu na kupoteza yote, huku wakikiacha kikosi kwa kocha, Jumanne Charles.
Tabora United waliachana na Kocha wao Mkuu Francis Kimanzi, Octoba 21, mwaka jana baada ya mwenendo usioridhisha wa timu hiyo.
Mkenya huyo alifurushwa pamoja na kocha wao msaidizi Yusuph Chipo.
Walimu hao waliiacha Tabora United wakiwa na pointi nane baada ya kucheza michezo nane, huku ikiwa ni wastani wa pointi moja kwa kila mchezo.

Baadaye Tabora walizinduka usingizini baada ya ujio wa Anicet Kiazayidi aliyembadili Kimanzi, na kuipaisha hadi nafasi ya tano wakiwa na pointi 33 kwa michezo 15 mwishoni mwa msimu.
Octoba 10, mwaka jana Kagera Sugar waliachana na Kocha Mkuu Paul Nkata na msaidizi wake Marwa Chamberi ambapo taarifa kutoka uongozi wa klabu hiyo ilidai mfululizo wa matokeo mabaya ndani ya kikosi hicho msimu huu ilikuwa sababu ya kuachana.
Baada ya kumtimua Nkata, Kagera Sugar ilimpa mikoba, Melis Medo raia wa Marekani na Misri kama Kocha wao Mkuu.
Raia wa Kenya, David Ouma wa Coastal Union mwanzoni mwa ligi hiyo aliachishwa kazi Agosti 23, huku kikosi kikiachwa kwa muda mikononi mwa Joseph Lazaro na Ngawina Ngawina.
Baadaye Octoba 22, wakamtangaza, Juma Mwambusi kuwa Kocha wao Mkuu.
Namungo pia, hawakuwa mbali na mdundo wa ngoma ya timua timua makocha kwani Octoba 24 mwaka jana walimbadilishia majukumu aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera na kuwa mshauri wa benchi la ufundi.
Nafasi yake ilichukuliwa na Juma Mgunda kama Kocha Mkuu akisaidiwa na Ngawina Ngawina, Shadrack Nsajigwa na Vladimir Niyonkuru.
Novemba 13, uongozi wa KMC ulithibitisha kwamba aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdihamid Moallin hatakuwa sehemu ya benchi lao la ufundi.
Pengo lake lilizibwa na Kali Ongala aliyetangazwa kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo tangu Novemba 14 mwaka jana.
Wakati huo huo Novemba 18, Yanga walimtambulisha, Moallin kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo.
Yanga nayo haikusalia nyuma, Novemba 15, iliachana na Kocha wao Mkuu Miguel Gamondi pamoja na msaidizi wake, Moussa Ndaw bila kuweka wazi sababu za kutoendelea nao.

Ikumbukwe wakati huo wenyeji hao wa mitaa ya Jangwani walipoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara wakifungwa bao 1-0 dhidi ya Azam FC na 3-1 na Tabora United.
Siku hiyo hiyo Novemba 15, baada ya Gamondi kupewa kisogo, alitambulishwa Sead Ramovic kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo.
Novemba 25, Singida Black Stars walitangaza kuachana na Patrick Aussems na msaidizi wake, Dennis Kitambi kwa kile walichokiita matokeo mabaya baada ya sare ya mabao 2-2 na Tabora United Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
Desemba 30 Singida BS walimtangaza mrithi wa Aussems kuwa ni Kocha Hamdi Miloud mwenye uraia wa nchi mbili za Ufaransa na Algeria akiambatana na wasaidizi wake, Nassim Anisse pamoja na David Ouma.
Desemba 28, 2024 Tanzania Prisons iliwashukuru aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo pamoja na msaidizi wake, Renatus Shija kwa kufikia makubaliano ya pande zote mbili kwa kusitisha mikataba yao ya kazi, kikosi kilikabidhiwa kwa kocha Shaban Mtupa.



