NaCoNGO yatoa wito kwa TRA kuhusu penati

BARAZA la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) Mkoa wa Iringa limeeleza jinsi linavyoumizwa na penati zinazotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati mashirika hayo yanapokumbwa na changamoto za kifedha.

Akizungumza katika kikao cha mashirika hayo kilichohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, Mjumbe wa NaCoNGO, Lediana Mng’ong’o, alieleza kuwa mashirika haya yamekuwa yakisaidia serikali kutoa huduma muhimu kwa jamii, lakini kwa sasa yanapitia kipindi kigumu cha kupungua kwa ufadhili na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.

Alisema hali hii imefanya mengi kushindwa kulipa kodi kwa wakati, na hivyo kukabiliwa na mzigo mkubwa wa penati zinazotishia kuyadhoofisha.

“Ukienda kule TRA, unaweza kukuta kila shirika linadaiwa kutokana na penati hizo, ambazo hutozwa wakati mashirika mengi yamesimamisha shughuli zake kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha,” alisema Mng’ong’o, ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa Viti Maalum (CCM) akiwakilisha mkoa wa Iringa.

Alisema NaCoNGO imependekeza TRA iangalie hali halisi ya mashirika haya na kutoa unafuu au msamaha wa penati wakati wa changamoto za kifedha.

Mwakilishi wa TRA aliyeshiriki kikao hicho, James Kagunda, alishauri mashirika yanayoshindwa kabisa kujiendesha kutokana na changamoto za kifedha yafikirie kufunga shughuli zake kwa muda mpaka pale yatakapopata rasilimali za kutosha.

“Kama ukifunga shughuli za ofisi na ukatoa taarifa TRA, mfumo wetu unaweza kufungwa na usiendelee kusoma taarifa za shirika. Kwa hiyo, ni bora kwa shirika kusimamisha shughuli zake kwa muda kuliko kuendelea kutozwa penati na kuzama zaidi kwenye madeni,” alisema Kagunda.

Aliongeza kuwa TRA iko tayari kushirikiana na mashirika hayo kutafuta njia za unafuu, huku akisisitiza umuhimu wa mashirika hayo kutathmini uwezo wao wa kuendelea na shughuli.

Wakati huohuo, mashirika hayo yametoa wito kwa serikali kutenga bajeti maalumu kuyasaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kupata rasilimali za kutekeleza miradi yao.

Walisema hatua hiyo inazingatia umuhimu wa mashirika hayo katika kuchangia maendeleo ya taifa, hasa katika sekta za afya, elimu, haki za binadamu, na mazingira.

Pia, mashirika hayo yametoa wito kwa serikali kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanapewa muda zaidi ya wanafunzi wengine wakati wakifanya mitihani yao.

Wamesema changamoto wanazokutana nazo wakati wa kufanya mitihani zimekuwa zikizorotesha matokeo yao, jambo linaloweza kuathiri mustakabali wao wa kielimu na kimaisha.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema takwimu za hadi Juni mwaka huu zinaonesha mkoa huo una jumla ya mshirika yasio ya kiserikali 321 na kati yake 85 hayana miradi.

Alisisitiza umuhimu wa mashirika hayo kutumia fedga wanazopata kwa kazi zilizokusudiwa na ambazo haziendani na mila, tamaduni na sharia za nchi.

Habari Zifananazo

Back to top button