SERIKALI imesistiza kuwa msukumo anautoa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na uwepo wa vyombo ya kiuwakajibikaji na serikali kuridhia Mpango wa Afrika wa Kujitathimini (APRM) kwa pamoja vinaendelea kuchochea uwazi hapa nchini.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi bungeni, Dodoma leo asubuhi wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega lililojikita katika uwazi.
Katika swali lake la msinmgi, Tendega amehoji sababu za serikali kujiondoa kwenye Mpango wa Uendeshaji wa Serikali kwa Uwazi (OGP) na katika maswali ya nyongeza, mwanasiasa huyo alitaka kujua lini serikali itarudi katika mpango huo.
Akijibu maswali hayo, Ndejembi alisema uwepo wa vyombo kama Tume ya Haki za Binadamu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na msukomo binafsi anaoutoa Rais wa Nchi kwa pamoja vinachangia uwazi na uwajibikaji.
“Mheshimiwa Spika, Uamuzi wa Serikali kujitoa OGP haujaathiri uendeshaji wa Serikali kwa uwazi kwa kuzingatia ukweli kwamba Serikali inao utaratibu wa ndani wa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na uendeshaji wa shughuli za Serikali kwa uwazi wakati wote kwa kuwa na vyombo na Taasisi zilizokasimiwa majukumu ya kusimamia na kufuatilia Sera ya Uwazi na Uwajibikaji. Mfano, TAKUKURU, Tume ya Haki za Binadamu…” amelieleza Bunge.
Amevitaja vyombo vingine vinavyochochea uwazi na uwajibikaji ni Utawala Bora, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tume ya Utumishi wa Umma.
Katika ngazi ya kimataifa, Naibu Waziri amesema kuwa Serikali imeendelea kuwa moja ya nchi zilizoridhia mfumo wa kukaguana wa nchi za kiafrika APRM (African Peer Review Mechanism) ambao ulianzishwa mwaka 2003 na Kamati ya Wakuu wa Nchi za Kiafrika.