Nassari achukua fomu ubunge Arumeru Mashariki

MWANZA: ALIYEKUWA Mkuu wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Joshua Nassari ni miongoni mwa wanachama 28 waliochukua fomu kuwania ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki lililopo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Nassari baada ya kuchukua fomu nje ya ofisi ya CCM Meru amesema kuwa ana uwezo wa kujenga hoja na kuwasilisha bungeni kutatua changamoto zinazowakabili wana Meru hivyo yeye sio mgeni bungeni bali anarudi kwa awamu ya pili kuendeleza alipoishia.

Amesema yeye ameombwa kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki na sio vinginevyo hivyo ana imani na chama chake na yuko tayari kutumwa kufanya kazi katika jimbo hilo kwa maslahi ya wananchi wa Jimbo hilo.

Mwana CCM mwingine aliyechukua fomu ni pamoja na Dk Mathew Mndeme ambaye amesema kuwa amekwenda kuwania ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kuwa ana udhoefu katika masuala ya uongozi na utawala.

Dk Mndeme amesema Jimbo la Arumeru Mashariki lina fursa nyingi lakini fursa hizo bado hazijawafaidisha wananchi wa jimbo hilo hivyo atatumia udhofu wake kunufaisha wananchi fursa zilizopo.

Mfanyabiashara maarufu jijini Arusha Hussein Gonga ni miongoni mwa wana CCM tisa waliochukua fomu kuwania ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini na hakuwa tayari kuzunguza chochote kwa madai kuwa muda ukifika atafanya hivyo ila kwa sasa hawezi kuzungumza chochote.

Nassari maarufu kwa jina la Dogo Janja akitinga ofisi za CCM Meru kuchukua fomu kuwani Ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki

Hata hivyo makatibu wa CCM Wilaya wamekatazwa kutoa majina ya watia nia ya ubunge baada ya kuagizwa kufanya hivyo na Katibu wa chama hicho ngazi ya Mkoa wa Arusha, Mussa Matoroka hata hivyo juhudi za kumsaka katibu kuelezea hilo zilishindika baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa.

Katika Jimbo la Longido, Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Steven Kiruswa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini ni miongoni mwa wana CCM sita waliochukua fomu kuwania tena nafasi hiyo na amefanikiwa kuirudisha leo kwa katibu wa chama hicho ngazi ya wilaya,George Kavenga.

 

Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ni miongoni mwa wana CCM wanaotarajiwa kuchukua fomu kesho jumanne katika ofisi ya chama hicho Jimbo la Arumeru Magharibi na Sabaya alipotafutwa amekiri kufanya hivyo kesho.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button