NBAA yaendelea kuwanoa wanafunzi taaluma ya uhasibu

DAR ES SALAAM: Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania (NBAA) imeendelea kutoa elimu na mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na shule za sekondari nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kukuza taaluma ya uhasibu na kuwajengea wanafunzi uelewa wa namna ya kujiunga na fursa zilizopo kupitia Bodi hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika wa NBAA, CPA Kulwa Malendeja, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, amekipongeza chuo kilichoshirikiana na Bodi hiyo kwa kuwaleta wanafunzi wanaosoma masomo ya uhasibu na biashara ili kupata elimu ya vitendo kuhusu kazi za NBAA.
CPA Malendeja amesema ili kuwa Mhasibu au Mkaguzi Hesabu aliyeidhinishwa kisheria, ni lazima mhitimu apitie mitihani ya NBAA na kupata cheti cha kitaaluma ambacho kinatambulika ndani na nje ya nchi.

Amesema vyeti hivyo vinafungua milango ya ajira na kutoa nafasi kwa wataalamu wa uhasibu kufanya kazi katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi pamoja na sekta ya kimataifa.
“Nimefurahishwa kuona hata wanafunzi wa Sheria wameshiriki katika ziara hii, kwani wana nafasi ya kusomea masomo ya uhasibu na kuwa CPA (Certified Public Accountant),” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya, amesema ziara za mafunzo ni fursa muhimu kwa wanafunzi kupata taarifa kuhusu huduma za NBAA na namna ya kujiandaa kitaaluma.
Ameongeza kuwa kutokana na maoni ya wadau, NBAA imeamua kuanzisha mahafali mawili kwa mwaka badala ya moja, ili kupunguza ucheleweshwaji wa utoaji wa vyeti vya kitaaluma kwa wahitimu.
Naye Dk Ayubu Timba, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro, ameishukuru NBAA kwa kuendelea kutoa elimu kwa wanafunzi na kueleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuwapa dira sahihi katika taaluma ya uhasibu.
Dk Timba pia amewataka wanafunzi waliopata elimu hiyo kuwa mabalozi wa taaluma yao kwa wenzao na jamii kwa ujumla.



