Ndolezi ACT kuzisemea changamoto za vijana

WAZIRI Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana chama cha ACT Wazalendo, Petro Ndolezi amesema nia yake kuunganisha vijana kusukuma agenda za ajira , mikopo ya elimu vyuo vya kati na vyuo Vikuu, kusimama na wajasiliamali na ushirikishwaji wa vijana kwenye vyombo mbalimbali vya maamuzi.

Akizungumza leo Februari 17, 2024 na HabariLEO, Ndolezi ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu anayewakilisha vyuo vikuu, amesema moja sababu zilizomfanya kuchukua fomu kugombea nafasi hiyo ni kuendelea kuwasemea vijana na kuwaunganisha kuwa kitu kimoja.

Ndolezi ameeleza kuwa kauli mbiu yake ni kuwa ‘Uongozi ni Kijiti’ na kwamba yupo tayari tayari kupokea kijiti kutoka kwa aliyemtangulia ili kuongoza ngome hiyo sambamba na kuendeleza mazuri na kuyatumia mapungufu kuweza kuboresha ngome.

“Vijana wa ACT Wazalendo wategemee ushirikiano na utendaji kazi wenye weledi na uwajibikaji. Watarajie kuyaona matumaini yao juu ya siasa za Tanzania na jamii kwa ujumla, pia kuifanya ngome kuwa jukwaa kimbilio la vijana wa Tanzania kwani tutakuwa tukipaza sauti juu ya changamoto za vijana”.amesema Ndolezi.

Akifafanua zaidi, Ndolezi amesema miongoni mwa vitu atakavyofanya endapo akipata nafasi hiyo ni kupaza sauti juu ya upatikanaji wa Baraza la Vijana la Taifa sambamba na kushawishi vijana wengi zaidi kujiunga na ACT Wazalendo.

Ndolezi aliyewahi kuwa Waziri Kivuli Sekta ya Maji na Mazingira amesema pia atahakikisha anaendeleza mazuri yaliyofanywa na kuboresha mapungufu yote ili kuongeza ufanisi wa ngome.

Habari Zifananazo

Back to top button