Ndolezi Petro kugombea ubunge Kigoma Kusini

KIGOMA: WAZIRI Kivuli Ofisi ya Waziri Mkuu-Bunge, Sera, Vijana, Kazi na Ajira wa Chama cha ACT Wazalendo Mhandisi Ndolezi Petro ametangaza rasmi nia ya Kugombea Ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini.
Mhandisi Ndolezi ametangaza nia hiyo katika mkutano wa hadhara wa kuzungumza na wananchi uliofanyika Kijiji cha Nguruka, Kata ya Nguruka Jimbo la Kigoma kusini.
Ameeleza pia msukumo wake wa kugombea nafasi hiyo umetokana na changamoto wanazopitia wananchi wa jimbo hilo.
“Jimbo la Kigoma Kusini linakumbwa na changamoto za miundombinu ya barabara, ukosefu wa pembejeo za kilimo, migogoro ya ardhi, huduma za afya kwenye vituo vya afya. Sera na mipango nitaeleza vizuri wakati wa kampeni nikipata ridhaa ya kugombea Jimbo la Kigoma Kusini,”ameeleza Petro.
Mhandisi Ndolezi Petro amekuwa mstari wa mbele kupigania agenda za vijana kupitia majukwa mbalimbali ikiwemo agenda ya Baraza la Taifa la Vijana, kujenga uchumi wenye kuzalisha ajira nyingi ili kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, anapigia chapuo pia uwepo wa mifuko ya hifadhi ya jamii jumuishi na sio tu kwa wale walio katika sekta rasmi ambao kwa Tanzania ni 9% ya nguvu kazi ya taifa na 91% hawapo kwenye hifadhi ya jamii.

Ikumbukwe kuwa Chama cha ACT Wazalendo kilifungua milango kwa watiania nafasi ya urais, ubunge na udiwani rasmi kupitia Katibu Mkuu wa Chama hicho, Ado Shaibu Januari, 15 2025.
Tangu pazia lifunguliwe kwa upande wa Urais hadi sasa waliotia nia ni wawili. Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyetangaza nia ni , Dorothy Semu ambaye kwa sasa ni Kiongozi wa Chama na kwa upande Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni , Othman Masoud Othman Sharif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Mkutano huo ameufanya kijijini kwao anakozaliwa na amewaomba wazee , vijana na akina mama kumuunga mkono katika safari yake.



