NEC yataka maelezo shida ya umeme, mafuta, bei mazao ya kilimo

HALMASHARI Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeelekeza kupatiwa ufumbuzi wa haraka wa kero ya kukatika kwa umeme, upungufu wa mafuta na changamoto ya bei ya mazao ya kilimo.

Hayo yamesemwa leo Desemba 1, 2023 na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, katika ziara yake mkoani Pwani kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.

“Chini ya Mwenyekiti Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kile kikao (NEC) kilifanyika siku nzima, mambo yote tuliyojadili ni yale yaliyohusu wananchi, tulijadili kuhusu kukatikatika kwa umeme, tatizo la mara moja moja la upungufu wa mafuta, tatizo la bei ya mazao; korosho, pamba, tumbaku, kahawa, alizeti na mengine yote,” amesena Kinana.

Advertisement

Amesema Rais Dkt. Samia alimtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kutoa majibu ya hoja zilizotoka kwa wajumbe wa NEC ambapo alifanya hivyo, akisaidiwa na mawaziri wakiwemo Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigilu Nchemba, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Kinana,amesema wajumbe wa kikao hicho walizungumzia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa upande wa Bara na Zanzibar.

Amesema, Mwenyekiti wa CCM Dkt. Samia, alimtaka Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa ilani.

Kinana amesema, changamoto zilizozungumzwa na wajumbe wa NEC kuhusiana na sekta mbalimbali zipatiwe ufumbuzi mapema iwezekanavyo kama alivyowahi kuagiza siku za nyuma.

“Mambo haya utekelezaji wake utafuatiliwa kwa karibu na Mwenyekiti mwenyewe, Rais Samia Suluhu Hassan ” alisisisitiza Kinana.

1 comments

Comments are closed.