NEC yawapiga msasa watendaji daftari la wapiga kura

TUME ya Taifa ya uchaguzi (NEC) imewajengea uwezo watendaji katika halmashauri tano za Simanjiro, Kiteto na Mbulu Mji sambamba na mikoa ya Singida na Dodoma katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Pia imewataka watendaji ngazi ya mkoa wanaoshiriki zoezi hilo kutunza vifaa vya uandikishaji ili viweze kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini.

Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi, Jaji Asina Omar amesema hayo September 14 katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi ya mkoa kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika jengo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, lililopo Wilaya ya Babati.

“Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa kutaathiri ukamilishaji wa zoezi hilo kutokana na vifaa kununuliwa kwa gharama kubwa,” amesema jaji Omar.
Amesema mafunzo yaliyotolewa yatawajengea umahiri wa kuwafundisha maofisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya kata ili waweze kutoa mafunzo kwa waendeshaji wa vifaa vya biometric na waandikishaji wasaidizi ambao ndio watahusika na uandikishaji wa wapiga kura kituoni.

Kwa upande wake ofisa mwandikishaji msaidizi jimbo la Mbulu Mji, Rehema Bwasi amebainisha kuwa vituo 113 katika kata 17 vimepokea vifaa na kuwahimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao.
Naye ofisa mwandikishaji msaidizi jimbo la Kiteto, Regina Loosunotia ameeleza kuwa wilaya hiyo imejipanga kufanya uboreshaji wa daftari la mpiga kura kuanzia Septemba 25 hadi Oktoba Mosi.




