NEC yawarejesha wagombea watatu udiwani

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imewarejesha wagombea watatu wa udiwani waliokuwa wameenguliwa kwa sababu mbalimbali.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa tume hiyo, Dk Wilson Mahera, imesema hatua hiyo ya kuwarejesha imekuja kutokana na rufaa walizozipitia, baada ya baadhi ya wagombea udiwani kutoridhika na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi kufuatia mapingamizi yaliyoweka katika uteuzi uliofanyika Novemba 30, 2022 Tanzania Bara.

Aliwataja wagombea ambao wamerejeshwa ni Joseph Machiya wa Chama cha  ACT-Wazalendo aliyerejeshwa kuwania Kata ya Mwamalili, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.

Mwingine aliyerejeshwa ni Vitali Maembe pia wa ACT-Wazalendo Kata ya Dunda, Halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo na Samwel Mnyellah wa NCCR-Mageuzi Kata ya Majohe, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

“Tume imefikia maamuzi hayo kwa kuzingatia Kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kikisomwa pamoja na kanuni ya 29(1), (2) na 30 (4) za Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani), 2020, ambavyo vinatoa fursa kwa wagombea Udiwani kukata rufaa wanapokuwa hawajaridhika na uamuzi wa Wasimamizi wa Uchaguzi kutokana na pingamizi zilizowasilishwa na vinaipa Tume mamlaka ya kukubali au kutengua uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi,” alisema Mkurugenzi wa Uchaguzi.

Uchaguzi huu Mdogo wa udiwani unafanyika katika kata saba ambazo ni Majohe (Dar es Salaam CC) Dar es Salaam, Mndumbwe (Tandahimba DC) Mtwara, Njombe Mjini (Njombe TC) Njombe, Dunda (Bagamoyo DC) Pwani, Mwamalili (Shinyanga MC) Shinyanga, Mnyanjani (Tanga CC) Tanga na Vibaoni (Handeni DC) Tanga.

Uchaguzi huo utafanyika sambamba na uchaguzi mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Amani, Wilaya ya Mjini, Zanzibar siku ya Jumamosi, 17 Desemba, 2022.

 

Habari Zifananazo

Back to top button