Nelly Msuya Kaimu Mkurugenzi MWAUWASA

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso amemteua Nelly Msuya kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).
Nelly amechukua nafasi ya Mhandisi Leonard Msenyele ambaye uteuzi wake umetenguliwa na Waziri Aweso jana August 20,2023.
Kabla ya uteuzi huo Nelly alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA).
Aidha; pamoja na uteuzi huo, Aweso ameunda timu ya wataalamu kutoka sekta ya Maji watakaofanyia kazi changamoto ya huduma ya maji kwa wakazi wa jiji la Mwanza sambamba na kusimamia kukamilika kwa mradi wa kuongeza maji katika mfumo wa usambazaji maji jiji humo.
Taarifa ya Aweso aliyoitoa leo Agosti 21, 2023 inasema kuwa timu hiyo aliyounda itaongozwa na wataalamu kutoka Wizara ya Maji makao makuu ambao ni Mhandisi Mkama Bwire, na Mkurugenzi wa Usambazaji Maji, Wakala wa Maji, Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Mhandisi Charles Mafie, Mkurugenzi Msaidizi Uendeshaji na Matengenezo, Wizara ya Maji.
Pia, timu hiyo ya wataalamu itahusisha wahandisi wengine ambao ni Nikas Mugisha, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma, Mhandisi Anthony Mayunga, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora, Mhandisi Valentine Njau, Meneja wa Miradi ya Majisafi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) na Mhandisi mwandamizi Ishmael Kakwezi, Mtaalamu wa Usimamizi wa Miradi.



