Ngajilo atikisa Iringa Mjini akichukua fomu

IRINGA: Mgombea Ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Ngajilo, amevuta macho na masikio ya wakazi wa mjini humo baada ya kuwasili kwa mbwembwe kuchukua fomu ya uteuzi kwa Afisa Uchaguzi wa Jimbo hilo, tukio lililoibua shamrashamra kubwa za kisiasa.
Ngajilo alitinga katika Ofisi za Uchaguzi zilizoko Halmashauri ya Manispaa ya Iringa majira ya saa 6.00 mchana, akisindikizwa na msafara mrefu wa bodaboda, magari na wananchi waliokuwa wakishangilia kwa nderemo na vifijo vilivyolitikisa eneo zima.

Baada ya kukabidhiwa fomu na Afisa Uchaguzi wa Jimbo, Robert Rumisha, Ngajilo alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mwenyezi Mungu, chama chake na wanachama wote wa CCM kwa imani waliyoonyesha kwake, akisema safari yake imejaa subira na mafunzo.
“Nawashukuru sana kwa mchakato ulionifikisha hapa. Hii ni mara yangu ya tatu kujaribu, safari ya kwanza na ya pili sikufanikiwa, lakini safari hii chama kimenipa imani kubwa na kuniteua. Ni heshima kubwa kwangu na nitailinda kwa nguvu zote,” alisema.
Akihimiza mshikamano ndani ya chama, Ngajilo alituma ujumbe mzito kwa wanachama akisema:
“Sina kundi zaidi ya kundi la CCM, tuvunje makundi. Tuwe kitu kimoja kuhakikisha ushindi wa chama chetu.”
Katika tukio hilo, Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, Hassan Makoba, alisisitiza kuwa chama hicho kiko tayari kupambana na mpinzani yeyote atakayesimama dhidi ya Ngajilo.

“Tutapambana na yoyote, awe sisimizi, mende au tembo; chama chetu kiko imara na mshikamano wetu ndiyo silaha kuu ya ushindi,” alisema Makoba huku akishangiliwa na umati wa wafuasi.
Ngajilo, ambaye ndiye mtia nia pekee aliyefika ofisini hapo kuchukua fomu kwa siku hiyo, ameahidi kampeni za kistaarabu zenye kushirikisha wananchi wote wa Iringa Mjini katika safari ya kuhakikisha CCM inabaki kuwa mstari wa mbele kwenye maendeleo ya jimbo hilo.


