Ngajilo kuboresha soko la mitumba Orofea Iringa

IRINGA:Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ameagiza kufanyika kwa maboresho ya haraka katika Soko la Mnada wa Mitumba Orofea, lililopo Kata ya Mshindo, Manispaa ya Iringa, ili kulifanya liwe rafiki zaidi kwa biashara na kuongeza tija kwa wafanyabiashara wanaolitegemea.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi sokoni hapo, Ngajilo amesema Iringa ni miongoni mwa miji inayokua kwa kasi kibiashara, huku biashara ya mitumba ikiajiri na kuhudumia mamia ya wakazi, hivyo mazingira ya soko yanapaswa kuendana na hadhi ya mji wa biashara.

Amesema changamoto za vumbi wakati wa kiangazi na tope kipindi cha mvua zimekuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli za kibiashara, hali inayopunguza mvuto wa soko kwa wateja na kuathiri kipato cha wafanyabiashara.

“Biashara haiwezi kukua bila mazingira bora. Soko hili ni chanzo cha kipato kwa familia nyingi, hivyo ni wajibu wa Serikali kuhakikisha linaendeshwa katika mazingira salama, safi na yanayovutia,” amesema Ngajilo.

Aidha, Mbunge huyo amesema eneo la jiko katika soko hilo halikidhi viwango vya utoaji huduma za chakula, jambo linaloathiri afya na ustawi wa wafanyabiashara, akisisitiza kuwa huduma za kijamii ni sehemu muhimu ya mnyororo wa biashara.

Ngajilo amesema kupitia Mfuko wa Jimbo, Serikali itaingilia kati kuboresha miundombinu ya soko hilo, ikiwemo sakafu, mifereji ya maji, eneo la jiko na upatikanaji wa maji safi, ili kuongeza ufanisi wa biashara ndogondogo na za kati.

Ameeleza kuwa ziara hiyo ni hatua ya awali ya tathmini, huku ukarabati ukitarajiwa kuanza ndani ya wiki tatu, na matarajio ni kwamba maboresho makubwa yatakuwa yamekamilika ifikapo mwezi wa pili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soko la Mnada wa Mitumba Orofea, Abuja Peter, amesema soko hilo lilijengwa na Serikali kwa lengo la kuwainua wananchi wa kipato cha chini na lina uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara zaidi ya 500 kwa wakati mmoja, endapo miundombinu itaboreshwa ipasavyo.

Mbunge Ngajilo pia amewaagiza wataalamu wa Manispaa ya Iringa kufanya tathmini ya haraka ya kitaalamu na kuwasilisha mpango wa maboresho ndani ya wiki mbili, ili utekelezaji uanze bila kuchelewa.

Katika ziara hiyo, amesisitiza umuhimu wa upatikanaji wa maji wa uhakika sokoni, akieleza kuwa maji ni nyenzo muhimu kwa usafi, afya na uendeshaji wa biashara.

Pia alitoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, inayogharimu Sh 150,000 kwa kaya yenye hadi watu sita, akihimiza wafanyabiashara kujilinda kiafya ili kulinda nguvu kazi yao.

Baadhi ya wafanyabiashara wamepongeza hatua hiyo wakisema ziara hiyo inaonyesha uongozi unaosikiliza wananchi na unaotambua mchango wa wafanyabiashara katika uchumi wa mji.

Naye Edina Sanga, fundi cherehani, amesema maboresho ya mabanda na eneo la jiko yatapunguza hasara wakati wa mvua na kuongeza ufanisi wa shughuli zao za kila siku.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button