MKUU wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amesema wamekamata zaidi ya ng’ombe 800 waliokutwa wakila katika mashamba na kuharibu mazao ya wakulima katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Alisema ng’ombe hao wamekamatwa kutokana na doria na oparesheni kubwa inayoendelea ya kuwaondoa wafugaji wote wanaofanya ufugaji na kuingiza mifugo kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.
Mtatiro alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kusisitiza kuwa ni lazima wafugaji wote kwenda katika vitalu vilivyotengwa kwa ajili ya kufugia badala ya kuendelea na ufugaji holela.
“Kuna tabia ya baadhi ya wafugaji kupeleka kwa makusudi mifugo yao kwenye mashamba na kuharibu mazao ya wakulima jambo linalosababisha migogoro mikubwa kati ya wakulima na wafugaji hao,” alisema.
Alisema mwaka 2019 serikali wilayani Tunduru ilitenga vitalu 250 ili vitumike kwa ajili ya ufugaji. Hata hivyo, ni vitalu 125 tu vimelipiwa na kutumika kwa ajili ya kazi hiyo.
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya alisema wamemkamata Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Machemba na Misechela na wenyeviti wa vijiji hivyo, kwa kuruhusu wafugaji kuingiza mifugo kwenye maeneo ambayo hayakutengwa kwa ajili ya ufugaji.