MFANYAKAZI wa eneo la machinjio jijini Hong Kong nchini China, amefariki alipokuwa akijaribu kuchinja nguruwe.
Mchinjaji huyo mwenye umri wa miaka 61 alimshtua nguruwe kwa umeme ili kumchinja lakini mnyama huyo akapata fahamu haraka, akajitenga na kumshambulia mtu huyo.
Katika harakati hizo, mchinjaji huyo aliangukia kisu cha sentimita 40 na kujeruhiwa vibaya kwenye mguu wake wa kushoto.
Madaktari walifika eneo la tukio na kumpeleka mchinjaji hadi hospitali, lakini haikuwezekana kuokoa maisha yake.
Polisi tayari wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo ili kubaini chanzo hasa cha kifo cha mfanyakazi huyo.
Wizara ya Kazi ya Hong Kong ilitoa salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na kusema kuwa imeanzisha uchunguzi wake kuhusu tukio hilo.
“Tutafanya uchunguzi haraka iwezekanavyo ili kubaini chanzo cha mkasa huo, kubaini waliohusika na kupendekeza hatua za kuboresha ulinzi wa wafanyakazi,” mamlaka ilisema kwenye taarifa.
Idara ya Chakula na Usafi wa Mazingira ya jiji hilo inayosimamia machinjio hayo pia ilitoa salamu za rambirambi kwa familia ya mchinjaji aliyefariki.
Kwa sasa haijajulikana ikiwa nguruwe huyo alifanikiwa kutoroka kuchinjwa.
Nguruwe mara chache huonesha uchokozi tu wakati wa kutetea nguruwe wenzao.
Wanasayansi wanaamini kuwa uwezo wao wa kiakili sio duni kuliko wanyama wengine wa nyumbani, hasa paka na mbwa. Wana kumbukumbu nzuri na hutumia takribani sauti 20 kwa mawasiliano.
Nguruwe pia anaweza kuitwa mmoja wa wanyama nadhifu zaidi. Ikiwa kuna mahali safi na kavu, hatalala kamwe kwenye uchafu.