NHC yatikiswa mradi wa Kawe 711

DODOMA — Ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha 2023/24 imebainisha kuwa miradi 24 ya ubia ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) haijakamilika kwa kipindi cha kati ya miaka 11 hadi 27, licha ya kuwa mikataba yake ilielekeza ikamilike ndani ya miaka miwili hadi mitatu.
Miradi hiyo ilikusudiwa kuendeleza viwanja muhimu vyenye majengo yasiyo na ubora ili kuzingatia mipango bora ya miji.
Licha ya hali hiyo, Shirika hilo limesaini mikataba mipya ya ubia 20 katika mwaka huo wa fedha, hatua ambayo CAG ameieleza kuwa inaleta hatari ya kufunga rasilimali kwenye miradi isiyo na tija.
Udhibiti dhaifu na usimamizi usioridhisha katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi umetajwa kama chanzo kikuu cha ucheleweshaji huo mkubwa.
CAG ameonya kuwa kuendelea kwa hali hii kunahatarisha ustawi wa Shirika kwa ujumla na kunadhoofisha matumizi bora ya rasilimali zake. Aidha, miradi iliyokwama inaziba nafasi ya kupata mapato ya muda mrefu kwa Shirika hilo.
Ametoa pendekezo kwa NHC kuhakikisha kuwa miradi iliyokwama inakamilika haraka kwa aidha Shirika lenyewe kuchukua usimamizi wake au kuhakikisha washirika wa maendeleo wanatimiza wajibu wao—vinginevyo walipe fidia ya hasara ya mapato yaliyopotea.



