NHIF yarejesha Toto Afya Kadi

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema kadi za huduma za watoto maarufu ‘Toto Afya’ zitaendelea shuleni na vyuoni baada ya kuondoa sharti la wanafunzi kujiorodhesha na kufi kia 100.

NHIF imeeleza kuwa kitakachohitajika sasa ni wazazi na walezi kusajili wanafunzi wao shuleni na watakaowahi
watahudumiwa katika kipindi kilichowekwa.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama wa mfuko huo, Hipoliti Lello wamesema hayo katika kikaokazi na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.

Advertisement

Dk Isaka alieleza kuwa Toto Afya ni eneo ambalo limekuwa na changamoto, ndiyo maana limefanyiwa uboreshaji.

Kwa mujibu wa Lello, sasa shule zitasajiliwa watoto kwa kuzingatia mwanzo wa masomo shuleni na vyuoni hata kama watakuwa 20 kati ya 80, basi hao wa mapema ambao wamelipa watapewa usajili na huduma kufuata.

“Tunafahamu kuwa kuna wazazi wengine wako na mwitikio wa haraka na wengine polepole. Sasa hata wanafunzi wakiwa 80 na wamejisajili haraka 20, kuanzia Januari hao watasajiliwa na kupewa huduma. Hao wengine watapewa huduma kwa kuzingatia muda uliokuwa umewekwa,” alisema Lello.

Lello alieleza kuwa mwitikio ni mkubwa na hadi sasa kazi hiyo inaendelea vizuri.

Awali, Toto Afya ilikuwa ikitumika kwa watoto wote lakini baadaye kadi hiyo ilisitishwa na kuwekwa kwa mfumo wa shuleni na vyuoni, kutokana na kuonekana gharama zake zimekuwa haziendani na uhalisia wa matibabu ya watoto.