‘Nida si lazima uboreshaji daftari wapigakura’

DAR ES SALAAM; TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imesema kitambulisho cha taifa au Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) si hitaji la lazima kwa mwananchi kujiandikisha kuwa mpigakura.

Aidha, wananchi wameondolewa wasiwasi kuhusu mfumo wa uandikishaji unaotumika na kusema hautakuwa na changamoto ya mtandao kwa sababu vifaa vitakavyotumika vina uwezo wa kutumiwa bila kuwa na mtandao wa intaneti.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Uandikishaji Wapigakura na Tehama wa INEC, Stanslaus Mwita katika mkutano wa tume hiyo na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu kuanza kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Akiwasilisha mada kuhusu mfumo wa uandikishaji wa wapigakura utakaotumika katika kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura 2024/25, Mwita alisema mifumo aina mbili itatumika. Mfumo wa kwanza ni mfumo mkuu uitwao (VRS) ambao umekuwa ukitumika katika uboreshaji wa daftari hilo tangu mwaka 2015/2020 na mfumo wa pili ni mfumo saidizi (OVRS) ambao umeanzishwa sasa kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa njia ya mtandao.

Alisema mifumo hiyo itahusisha matumizi ya NIN ambayo inatolewa na Nida na kuwa mifumo hiyo inaweza kuvuta taarifa za mamlaka iwapo mpigakura atakuwa na namba ya kitambulisho hicho, hivyo kurahisisha uandikishaji.

“Tunasisitiza namba ya utambulisho wa taifa ya Nida si hitaji la lazima katika kumwandikisha mpigakura, hivyo wananchi ambao hamna msiache kwenda kujiandikisha ili mradi umekidhi vigezo,” alisema.

Kuhusu wasiwasi wa kukwama kwa mtandao wakati wa kujiandikisha, Mwita alifafanua kuwa tume imejipanga vizuri kuhakikisha hakuna changamoto ya uandikishaji wapiga kura kwenye mfumo kwa kuwa vifaa wanavyotumia vina uwezo wa kuandikisha bila kuwa na mtandao.

Alisema kwa jiografia ya nchi, vijiji vingi nchini havina miundombinu ya Tehama na kuwa vifaa wanavyotumia vya bayometriki vimewekwa mfumo ambao muda wote unaweza kuingiza taarifa za mpigakura bila kujali kama kuna mtandao au la.

“Kuhusu mtandao na vifaa vyetu wananchi wasiwe na wasiwasi, vina uwezo wa kuchukua taarifa za mpigakura na kuzihifadhi hata kama hakuna mtandao, alafu baadaye tukifika maeneo yenye mtandao taarifa zinajituma na kuendelea kuhifadhiwa,” alisema.

Akijibu swali kuhusu kuondolewa kwa watu waliokosa sifa kwenye daftari hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima alisema wapigakura 594,494 wanatarajiwa kuondolewa kwenye daftari hilo kwa kukosa sifa. Alifafanua kuwa kukosa sifa za kuendelea kuwa mpiga kura ni pamoja na mtu kufariki dunia, kubadili uraia na sifa nyingine.

Utaratibu wa kumwondoa hufanywa kwa kufuata hatua na ngazi ya mwisho ni kumfuta mtu huyo ni kwa idhini ya mkurugenzi wa uchaguzi wa INEC.

Kailima alisema daftari la wapiga kura litawekwa wazi kwenye maeneo ya kata husika na wananchi wanapita kukagua. Wanaweza kutoa taarifa za kifo cha mpigakura na ambaye atakuwa amepoteza sifa za kuendelea kuwapo.

“Utaratibu unatumika kuanza kumwondoa kwa kuleta nyaraka zinazothibitisha kifo na hatua zitaendelea hadi kujiridhisha na kumuondoa,” alisema.

Kuhusu muda utakaotumika kwa mpigakura mmoja kuboresha taarifa zake kituoni hapo, Mwita alisema hautazidi dakika tatu hadi nane kwa kuwa vifaa hivyo vimewekewa mifumo ya kisasa kuchakata na kuhifadhi taarifa.

Katika uboreshaji huo wa Daftari la Wapiga Kura litakalozinduliwa rasmi Julai Mosi, mwaka huu, zaidi ya wapiga kura wapya milioni 5.58 wanatarajiwa kuandikishwa.

Hao ni sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura zaidi ya milioni 29.75 waliopo kwenye daftari hilo kwa uboreshaji wa mwaka 2019/2020. Aidha, INEC inatarajia wapiga kura zaidi ya milioni 4.4 wataboresha taarifa zao na hivyo baada ya uboreshaji wa 2024/2025, INEC inatarajia daftari hilo liwe na wapiga kura zaidi ya milioni 34.74.

Habari Zifananazo

Back to top button