NIDA wakabidhi gawio Sh bilioni 61 serikalini

DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imekabidhi Serikalini Sh bilioni 61.05 ikiwa ni makusanyo yake ya mwaka, huku ikishika nafasi ya pili miongoni mwa taasisi za umma zilizofanya vizuri katika kuwasilisha gawio na michango kwa Serikali.

Fedha hizo zenye thamani ya Sh 61,053,535,363 zilikabidhiwa kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika hafla ya upokeaji wa gawio na michango ya taasisi za umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam, Juni 30, 2026.

Mbali na kukabidhi mchango huo, NIDA ilitunukiwa tuzo ya nafasi ya pili kwa kutambua mchango wake katika kuongeza mapato ya Serikali na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema mafanikio hayo yametokana na kuendelea kuimarishwa kwa mifumo ya utoaji huduma za utambuzi wa taifa.

Amesema mchango huo unaonyesha matokeo ya maboresho ya huduma za utambuzi ambazo zimeendelea kuimarisha usalama wa nchi, kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kuchochea ongezeko la mapato katika sekta za umma na binafsi.

Kaji alisema NIDA itaendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la kusajili na kuwatambua wananchi kwa kutoa Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN) na Vitambulisho vya Taifa, pamoja na kuwezesha matumizi ya taarifa sahihi za utambuzi katika sekta mbalimbali.

Alieleza kuwa mfumo wa utambuzi wa taifa ni nguzo muhimu katika kuboresha upangaji na utoaji wa huduma kwa wananchi, kuimarisha usalama, kudhibiti udanganyifu na kuongeza ufanisi katika sekta za umma na binafsi.

Aidha, NIDA imeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza na kuimarisha mifumo ya utambuzi nchini, huku ikitoa shukrani kwa wananchi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa katika kujenga taifa lenye utambuzi sahihi na huduma bora.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button