Niffer, wenzake 21 kortini wakituhumiwa uhaini

DAR ES SALAAM; MFANYABIASHARA Jeniffer Jovin, maarufu ‘Niffer’(26)na wenzake 21wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakibabiliwa na makosa matatu yakiwemo ya uhaini.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwalimu, Lucianus Luchius (28), Paul Malima (28), Augustino Mulwale (30), Mohamed Kondo (30), John Mmena (26), Paul Shirima (23), Ramadhani Ramadhani (21), Levi Mkute (40), Esau Ernest Maarufu ‘Duduye’ (21), Leonard Mkonyi.
Pia wapo Fadhili Nyombi, Hamisi Hamisi, Abeid Kivuyo (24), Nicholous Shiduo (27),Abati Mwadini (27) Mika Chavala (32), Fatuma Mzengo (30), Dewji Ramji (19), Ruthmelda Silaa (21), Hilda Ngulu(22) na Yusuph Hussein(22).
Jopo la Mawakili wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Clemence Kato waliwasomea washitakiwa hao makosa yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya washitakiwa walipofikishwa mahakamani hapo.
Akiwasomea washitakiwa mashitaka yao Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato alidai washitakiwa wanakabiliwa na makosa matatu mbkele ya mahakama hiyo la kwanza likiwa ni la kupanga njama na mengine mawili ni ya uhaini.
Wakili Kato alidai katika tarehe tofauti kati Aprili 15, 2025 na Oktoba 29, 2025, katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam,walikula njama na kupanga kwa siri kufanya kosa la uhaini.
Aliendelea kudai kuwa shitaka la pili lilimuhusisha mshitakiwa wa pili hadi 21, ilidaiwa Oktoba 29, 2025, katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wakiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliunda nia ya kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Alidai washitakiwa walifanya hivyo kwa lengo la kutishia mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na walionyesha nia hiyo kwa kusababisha uharibifu mkubwa wa mali za Serikali zinazokusudiwa kutoa huduma muhimu.
Wakili Kato alidai shitaka la tatu linamuhusu Niffer peke yake ilidaiwa kati ya Agosti 15,2025 hadi 24 Oktoba 24,2025, katika maeneo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, akiwa chini ya utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku wakiwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliunda nia ya kushawishi umma kuzuia Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Alidai mshitakiwa alifanya hivyo kwa lengo la kutishia mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na walionesha nia hiyo kwa kuhamasisha umma kununua barakoa kwa ajili ya kujikinga na mabomu ya machozi katika biashara yake.
Alidai ili kujilinda na mabomu ya machozi ya polisi wakati wa maandamano yasiyo halali yaliyoashiria kusimamisha Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Baada ya washitakiwa kusomewa makosa yao Hakimu Lyamuya alisema washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haikuwa na mamlaka ya kusikiliza makosa ya uhaini.



