NIT kufundisha watalaamu wa mazingira vyombo vya moto

DAR ES SALAAM: KATIKA kuadhimisha wiki ya mazingira duniani, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwafundisha wataalamu wa usafiri waliobobea katika kulinda mazingira, hasa kwa kuzingatia athari zitokanazo na vyombo vya moto kama magari, malori na pikipiki.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Idara ya Usafiri Salama na Uhandisi wa Mazingira Mhandisi Patrick Makule amesema sekta ya usafiri ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya uchafuzi wa hewa kutokana na utoaji wa gesi chafu, hivyo ni muhimu kwa wataalamu wa fani hiyo kufundishwa namna ya kupunguza madhara hayo.
“Tunawajengea wanafunzi wetu uelewa mpana kuhusu usafiri endelevu, matumizi ya teknolojia safi, na umuhimu wa kuzingatia viwango vya kimazingira katika uhandisi wa usafiri,” amesema Mhandisi Makule.
Aidha, Mhandishi huyo amesema kuwa NIT imejikita katika kutoa elimu ya vitendo na tafiti zinazolenga kuboresha mifumo ya usafiri ili iwe salama kwa binadamu na rafiki kwa mazingira.
Kwa mujibu wa NIT, hatua hii ni sehemu ya juhudi za kitaifa na kimataifa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda afya ya jamii.
Kwa upande wa serikali kupitia Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis, amepongeza Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa jitihada zake za kuwawezesha vijana wa Kitanzania na kwa kuoanisha sekta ya usafirishaji na mazingira kwa namna endelevu.
Akizungumza jijini Dodoma alipotembelea maonesho ya Wiki ya Mazingira, Khamis alisema kuwa mchango wa taasisi za elimu kama NIT ni muhimu katika kuhakikisha vijana wanapata elimu stahiki itakayowasaidia kushiriki katika maendeleo ya Taifa bila kuathiri mazingira.
Ameeleza kuridhishwa na ubunifu wa NIT katika kushughulikia changamoto za mazingira kupitia elimu ya usafirishaji rafiki kwa mazingira. Aidha, alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi kama NIT ili kuimarisha usawa wa maendeleo na uhifadhi wa mazingira.
Naibu Waziri Hamza alikuwa ameongozana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula.