Nitamaliza vita vya Urusi na Ukraine – Trump

MAREKANI : RAIS mteule wa Marekani, Donald Trump, amepanga kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, mara baada ya kuapishwa kwake Januari 20, kwa lengo la kujadili juhudi za kumaliza vita vya Urusi na Ukraine.
Akizungumza na waandishi wa habari huko Florida, Trump alisisitiza kuwa anatarajia kumaliza vita hivyo ndani ya kipindi cha miezi sita, akieleza kuwa ataweka kipaumbele katika kutafuta suluhu ya amani kupitia mazungumzo.
Trump alikumbusha ahadi aliyotoa wakati wa kampeni zake, ambapo alisema angeweza kumaliza vita hivyo ndani ya saa 24. SOMA : Zelensky: Trump anaweza kumaliza vita na Urusi
Hata hivyo, vita vya Urusi na Ukraine vimeingia mwaka wa tatu sasa, na hali ya kiusalama inazidi kuwa tete.
Ukraine inahofia kwamba, ikiwa Trump atachukua madaraka, msaada wa Marekani kwa nchi hiyo unaweza kupungua, jambo ambalo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, alikazia katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, akiiomba Washington kutopunguza msaada wa kijeshi na kifedha kwa Ukraine.
Trump aliendelea kusema kuwa atafanya kila liwezekanalo kumaliza mzozo huu wa kivita kwa njia ya mazungumzo, badala ya kutegemea hatua za kijeshi.
Taarifa hii imezua mjadala mkubwa duniani, huku wakosoaji wakidai kuwa utekelezaji wa ahadi hiyo unaweza kudhoofisha usalama wa Ukraine, lakini wafuasi wa Trump wakisema kuwa ni njia bora ya kudumisha amani na kuzuia uharibifu zaidi.