BENKI ya NMB imeahidi kuendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhakikisha usawa wa kijinsia katika sekta ya kibenki nchini, ikiwa ni ahadi ya benki hiyo kuunga mkono uchumi sawa na uliowezeshwa.
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la International Finance Corporation (IFC) mkoani Dar es Salaam jana kujadili mafanikio ya mradi wa ‘Finance2Equal’ kwa wadau wake, Ofisa Mkuu Rasilimali Watu wa Benki ya NMB, Emmanuel Akonaay alisema benki yake kwa muda mrefu imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha usawa wa kijinsia mahala pa kazi.
Akonaay alisema bila ukuaji jumuishi wa kijinsia, kufikia ukuaji wa muda mrefu wa kiuchumi itabaki kuwa ndoto.
“Utafiti unaonesha kuwa uwiano wa kijinsia unaweza kuchochea ukuaji wa kiuchumi, kuimarisha uchumi na utulivu kifedha na uwiano wa kipato,” alisema.
Alisema tayari benki yake imepiga hatua kubwa katika suala zima la kuongeza uwiano wa usawa wa kijinsia na kusema katika benki hiyo, uwiano wa kijinsia umepanda kutoka asilimia 45 wanawake, asilimia 55 wanaume mwaka 2015 na kufikia asilimia 49 wanawake, asilimia 51 wanaume mwaka huu.
“Ahadi yetu juu ya uwiano wa kijinsia haishii tu kwa wafanyakazi wetu wa ndani ya benki bali hata kwa wanawake tunaowahudumia kwenye soko letu,” alisema.
Alisema Februari mwaka huu benki yake ilitoa hati fungani ya kipekee na ya kwanza kutokea kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki almarufu kama ‘Jasiri Bondi’ ambayo ilisaidia upatikanaji wa Sh bilioni 74.2 ambazo zitatumika kutoa mikopo nafuu kwa wajasiriamali wanawake au biashara za wanawake na zile ambazo zinagusa wanawake moja kwa moja.
“Ili kuchangia ushiriki wa wanawake kwenye sekta za kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na uchumi wa buluu, benki yetu ilitenga Sh bilioni 100 kuendeleza mnyororo wa thamani kwenye sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka. Hata hivyo, tuliweza kuchangia shilingi bilioni 100 za ziada kwa riba ya asilimia tisa kwa mwaka,” alisema.
Akonaay alisema nchini kwa sasa wanawake wengi wanakosa fursa za kifedha kutokana na kutengwa na mifumo mingi ya kifedha hali ambayo inaathiri uchangiaji wao kwenye shughuli za kiuchumi.
“Kupitia hati fungani yetu ya Jasiri ambayo inalenga makundi mbalimbali ya wanawake, benki yetu imeendelea kuwa mstari wa mbele kuwezesha wanawake na hadi Juni mwaka huu, benki imetoa mikopo 1,483 yenye thamani ya shilingi bilioni 35 kuwezesha biashara zinazomilikiwa na wanawake,” alisema.
Awali, Mwakilishi Mkazi wa IFC nchini Tanzania, Frank Ajilore alisema uwekezaji kwa wanawake kupitia ajira, uongozi, ubunifu ni muhimu na unasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Kwa miaka kadha iliyopita kwa mfano wateja wetu kutoka taasisi za kibenki 150 ilibaini kuwa mikopo chechefu kwa wanawake ilikuwa asilimia 3.6,” alisema.
Akitoa ripoti mradi wa Finance2Equal, Anna Casanova, Mtaalamu wa masuala ya kijinsia wa IFC alisema kupitia utafiti wao, wakurugenzi wa kampuni mbalimbali walisema kuwa wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa uendeshaji na ushindani.