MWENYEKITI wa Ngome ya Vijana wa chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo ametangaza nia ya kugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika Februari 29, 2024.
Nondo ametoa taarifa hiyo leo Februari 5, 2024 kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii ambapo pia amewataka vijana wenzake wa chama hicho kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali.
“Ninawaomba na kuwasihi sana vijana ndani ya chama chetu mjitokeze kugombea nafasi zilizopo hasa nafasi hii ya uenyekiti wa Ngome na Makamu Mwenyekiti Taifa ili wajumbe wawe na machaguo mengi zaidi.” Ameandika Nondo.
Amesema uchaguzi huo utakuwa katika nafasi za Mwenyekiti wa Ngome Taifa na Makamu Mwenyekiti Taifa hata hivyo itafuatiwa na uchaguzi wa Ngome ya Wazee Machi 1, 2024, na uchaguzi wa Ngome ya Wanawake Machi 2, 2024.
Nondo amesema uchaguzi wa kuchagua viongozi wakuu wa chama ACT Wazalendo kama kiongozi wa chama, Mwenyekiti wa chama na Makamu Mwenyekiti wa chama itakuwa tarehe Machi 5, 2024 na itafuatiwa na mkutano wa hadhara wa kutangaza viongozi wapya waliochaguliwa ambao utakuwa Machi 6, 2024. Amesema zoezi la kuchukuaji na kurejeshaji fomu ni kuanzia Februari 14-24, 2024.