Norway yaguswa huduma afya ya uzazi 

Norway yaguswa huduma afya ya uzazi 

SERIKALI ya Norway imeitaja Tanzania, kuwa miongoni mwa nchi itakayofikia maazimio ya kimataifa ya kuhakikisha haki ya upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi, kabla ya mwaka 2030.

Hatua hiyo imetokana na juhudi za serikali hususan utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan  la kusimamia haki ya usawa, kwa kuwarudisha shuleni wasichana waliokatisha masomo sababu ya mimba.

Akizungumza na wadau mbalimbali wa afya ya uzazi Dar es Salaam, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Norway, Anne Tvinnereim’s, amesema wanaamini Tanzania itafika mbali zaidi katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi (SRH), ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa.

Advertisement

Amesema kuwa ushirikiano baina ya nchi ya Tanzania na wadau wa maendeleo, sambamba na uwepo wa utayari wa kisiasa kumesaidia kuleta mafanikio makubwa katika utekelezaji maazimio hayo.

“Tutaendelea kuisapoti Tanzania, kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA),  kuhakikisha tunaboresha afya ya uzazi, hususan kwa vijana, kwani wanahitaji taarifa zaidi za afya ya uzazi na namna ya kupanga maisha yao, ili kufikia malengo,” amesema Tvinnereim’s.

Ameeleza kuwa haki ya kufanya maamuzi kuhusu afya ya uzazi, huwezesha watu kuishi maisha yao kwa uhuru  na kwamba upatikanaji wa SRH ni moja ya maeneo  ambayo yanaweza kuboresha nafasi za wanawake na wasichana kupata elimu, kwa kuwasaidia wanawake kushiriki katika ajira na kuboresha mapato.

Naye  Mwakilishi Mkazi wa UNFPA, Mark Schreiner,  amesema serikali ya Tanzania imefanikiwa katika kuongeza huduma za afya ya uzazi kwa mama, watoto na vijana balehe.

Pia amesema imeweka sera na malengo ya kuboresha huduma za afya, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya.

“Mwaka 2021 zaidi ya watoto milioni mbili walizaliwa sawa na asilimia 44 ya idadi ya watu wenye umri wa miaka 15. Uwekezaji mkubwa unahitajika kuboresha huduma za afya ya uzazi, uzazi wa mpango na kuzuia mimba za utotoni,” ameeleza Schreiner.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Watoto kutoka Wizara ya Afya, Dk Ahmad Makuwani, amesema kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuimarisha afya ya uzazi, kwani kuna ongezeko la watumiaji wa uzazi wa mpango na kutoa chanjo ya kujikinga na saratani kwa wasichana wenye umri chini ya miaka 18.

Amesema mikataba mingine wanayoitekeleza ni wa Maputo ambao pamoja na mambo mengine unaelekeza kupunguza mimba na ndoa za utotoni.