MFUKO wa Hifadhi ya Jamii Taifa (NSSF) Mkoa wa Kahama umetoa vyeti kwa waajiri 15 kutoka kampuni na zahanati na shule binafsi wanaochangia vizuri kwenye mfuko huo wakiongozwa na Kampuni ya Barrick Bulyanhulu Gold Mine inayochangia Sh bilioni 1.5 kwa wanachama 1380.
Meneja wa NSSF Kahama, Aisha Nyemba amekabidhi vyeti hivyo leo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Wateja yaliyoanza Oktoba 7, 2024 ambapo kauli mbiu ikiwa ‘Huduma Bora Popote Ulipo’
Nyemba amesema mchangiaji wa pili mzuri kwenye mfuko huo ni Kampuni ya MS Laboratories Ltd ambaye anachangia Sh milioni 50 kwa mwezi akiwa na wanachama 102.
Nyemba amesema Kampuni ya Msalala Gold Limited yenye wanachama 62 na anachangia Sh milioni 9 kwa mwezi huku akitaka waajiri wengine kuchangia kwa wakati.
Aidha katika kundi la wanachama binafsi aliwataja watu watano wanaochangia vizuri kila mweizi katika mfuko huo huku akiwataka na watu wengine wajiunge ili waweze kufaidika na matibabu katika hospitali zote hapa nchini.
“Sasa hivi Kuna mfumo uliowekwa wa kujisajili,kulipa mchango wako, kuangalia kiwango ulichochangia ukiwa huko huko eneo lako la kazi au biashara bila kufika ofisini na kupoteza muda,”amesema Nyemba
Ofisa mwandamizi sekta isiyorasmi Magreth Mwaibasa amesema mfuko huo ulikuwa unahusisha Serikali sasa watu binafsi kama wajasiriliamali nao wanastahili kuchangia upo utaratibu uliowekwa kwao hivyo wasisite kujiunga