Nusu fainali Angeline Jimbo Cup kupigwa leo
MASHINDANO ya Angeline Jimbo cup yanatarajia kuendelea leo jioni kwa mchezo mmoja wa nusu fainali kati ya kata ya Kirumba dhidi ya Nyakato katika uwanja wa shule ya msingi Saba saba wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Mchezo wa pili wa nusu fainali utachezwa kesho katika uwanja huo huo kati ya kata ya Shibula dhidi ya Ibungiro.
Akizungumza na HabariLEO, Kocha mkuu wa timu ya Nyakato Smith Swai amesema timu yao imejipanga kuweza kupambana na kupata ushindi ili waweze kufuzu na kuingia hatua ya fainali.
Naye Katibu wa mbunge wa jimbo la Ilemela,Charles David ameziomba timu zote zilizoingia nusu fainali zijitaidi kucheza mchezo safi.
Amesema mshindi wa mashindano hayo atapokea fedha taslimu Sh milioni 2.5 pamoja na kikombe huku nafasi ya pili atapokea Sh milioni 2.
Amesema nafasi ya tatu atapokea Sh milioni 1.5 huku nafasi ya nne atapokea Sh milioni 1.
Amesema kwa upande wa timu yenye nidhamu na timu ya mashabiki bora zote zitapokea shilingi 500,000/- kwa kila timu.
Amesema mwamuzi bora na mwandishi bora watapokea Sh 300,000 huku mchezaji bora atapokea shilingi 200,000/-.