Nyalusi autaka tena ubunge viti maalum Iringa

IRINGA: MBUNGE wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa anayemaliza muda wake, Nancy Nyalusi, amechukua rasmi fomu ya kuomba ridhaa ya kuendelea kulitumikia Taifa kupitia nafasi hiyo ya uongozi.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tu tangu kuanza kwa zoezi la kuchukua fomu kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, huku Nyalusi akisisitiza dhamira yake ya kuendeleza mapambano ya kuwakwamua wanawake, wasichana na makundi mengine ya pembezoni.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo, Nyalusi alitoa shukrani kwa wanachama na viongozi wa CCM kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kulitumikia Taifa kwa miaka mitano iliyopita, akiahidi kuwa endapo atapata ridhaa tena, ataendeleza juhudi zake za kupaza sauti za wanawake katika ngazi zote.
“Nawashukuru viongozi na wanachama wangu, kupitia kwa Mwenyekiti wetu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan. Niliaminiwa na kupewa nafasi hii. Nimeitumikia kwa miaka mitano na sasa nimechukua fomu kutetea tena ili niendelee kuwatumikia wananchi na chama changu,” alisema.
Nyalusi anatajwa na wengi kama kielelezo cha mwanamke shupavu, ambaye katika kipindi cha miaka mitano aliyohudumu amejikita kwenye ajenda ya kutetea makundi maalumu na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, elimu kwa wasichana, na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Katika harakati zake, amekuwa mstari wa mbele kusukuma ajenda za usawa wa kijinsia bungeni na kwenye jamii, huku akiendesha kampeni za uelimishaji kwa wanawake wa vijijini kuhusu fursa mbalimbali za maendeleo zinazopatikana kupitia serikali na mashirika binafsi.
Kwa maono na msimamo wake, Nancy ameendelea kuwa sauti ya matumaini kwa wanawake wa mkoa wa Iringa, akiwaonesha kuwa nafasi za uongozi zinaweza kufikiwa kwa bidii, nidhamu, na kujituma.