NYAMOGA: Nyomi za Dk Samia ni ushahidi wa mapinduzi ya kisiasa

IRINGA: Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga, amezungumzia wingi wa wananchi waliojitokeza kumsikiliza mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan, akisema nyomi hizo si za kawaida bali ni alama ya mapinduzi makubwa ya kisiasa yanayoshuhudiwa nchini.
Akizungumza mara baada ya mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja wa Samora, mjini Iringa, Nyamoga alisema umati huo ni sauti ya wananchi wanaoonesha namna walivyoguswa na kazi za Rais Dk Samia katika awamu yake ya kwanza, hususan miradi mikubwa ya maendeleo inayolenga kumuinua mwananchi wa kawaida.
“Mkiangalia nyomi hizi ni kielelezo cha mapokezi ya kazi nzuri alizofanya Rais wetu. Watanzania wameona mabadiliko, wameona uongozi wenye dira, ndio maana wanasimama bega kwa bega kuunga mkono awamu ya pili,” alisema Nyamoga.
Hata hivyo, alikiri pia kuwa safari yake kisiasa ndani ya CCM imepata changamoto baada ya jina lake kutoorodheshwa na Kamati Kuu ya chama hicho kuwania ubunge wa Kilolo mwaka huu.

Lakini, kwa maneno yenye utulivu wa kisiasa, Nyamoga alisema: “CCM ina hazina kubwa ya wanachama wenye uwezo wa kugombea, kwa hiyo hili sio mwisho wangu kisiasa. Mapambano yanaendelea.”
Kuhusu hoja ya vyama vya upinzani kudai CCM haina mpinzani wa kweli mwaka huu, Nyamoga alijibu kwa msisitizo: “CCM si chama cha kujipima yenyewe. Kinashindana na zaidi ya vyama 15 vilivyosimamisha wagombea. Hata pale ambapo hakuna mgombea wa upinzani, mgombea wa CCM anapigiwa kura ya ‘ndiyo’ au ‘hapana.’ Hiyo ndiyo taswira mpya ya demokrasia nchini.”
Kauli hiyo ya Nyamoga imechukuliwa na wachambuzi wa siasa kama ujumbe wa kujenga ari kwa wanachama wa CCM na kuibua hoja mpya kwa wapinzani wanaodai uchaguzi hauna mizani ya kisiasa.


