Nyerere na teknolojia kama msingi wa uchumi wa kujitegemea

IKIWA imepita miaka 26 tangu kifo cha Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere bado viongozi wa Tanzania wanaendelea kuyaishi mawazo, falsafa na busara zake kuiongoza nchi.
Miongoni mwa maono hayo ni nchi kutumia teknolojia kukuza uchumi na kuzalisha bidhaa zake kwa kutumia viwanda vya ndani ili kujiimarisha na kujitosheleza kwa bidhaa za ndani badala ya kutegemea za nje.
Katika kupambana na maadui wakubwa watatu; ujinga, umaskini na maradhi baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967, Nyerere alianzisha viwanda ili kutumia teknolojia kuongeza thamani ya mazao ya ndani vikiwemo viwanda vya nguo vya Urafiki, Sungura na Mwanza Textile (Mwatex).
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania (SAUT) na mtaalamu wa uchumi, Dk Isaac Safari anasema serikali chini ya uongozi wa Nyerere ilifanikiwa kutumia teknolojia kuanzisha viwanda mbalimbali vikiwamo viwanda va usindikaji chakula na maziwa na viwanda vya saruji Tanga na Mbeya ambavyo vilihusisha teknolojia za uzalishaji zilizoagizwa kutoka nchi rafiki kwa asilimia ndogo.
Katika mazungumzo na gazeti HabariLEO kuhusu kumbukizi ya miaka 26 tangu kifo cha Nyerere, Dk Safari anasema Nyerere aliamini kilimo ndicho kiini cha uchumi wa Tanzania. Anasema ndiyo maana kiongozi huyo alisisitiza kilimo cha kisayansi kupitia matumizi ya trekta na zana za kisasa kwenye mashamba ya vijiji vya ujamaa na wakati wote aliamini katika teknolojia kwenye kilimo.
Anasema Dk Safari, “Mwalimu Nyerere alianzisha taasisi za utafiti wa kilimo mfano Ilonga, Uyole na Ukiriguru ili kutumia teknolojia kuboresha mbegu, mbolea na mbinu bora za kilimo.” Anaongeza: “Mengine ni uanzilishi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na mashirika mengine yalihamasishwa kuwekeza katika kilimo cha miwa, chai, tumbaku na pamba kwa kutumia mashine na viwanda vya kuchakata’’.
Anasema serikali chini ya uongozi wa Nyerere ilijitahidi kutumia teknolojia ya nishati na miundombinu mbalimbali
ikiwemo mradi wa Mto Kiwira (Mbeya) na Mtera Hydropower ulioanza kufanyiwa maandalizi wakati wa uongozi
wake ili kuongeza upatikanaji wa umeme nchini.
Anasema Nyerere alihimiza barabara, reli na mawasiliano kwa kutumia teknolojia ya ujenzi kurahisisha biashara. Mfano mkubwa ni Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA). Katika sekta ya elimu, Dk Safari anasema Nyerere alisisitiza elimu ya kujitegemea. Shule na vyuo vikuu vikahamasishwa kutumia teknolojia rahisi kwenye kilimo na ufundi stadi.
Kwa mfano Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kilianzishwa kama kitovu cha teknolojia na utafiti. Anaeleza kuwa Nyerere alianzisha vituo vya ufundi na mamlaka kama Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ilitokana na dhana ya kuandaa vijana kutumia teknolojia kujitegemea.
Dk Safari anasema hata katika sekta ya afya, Nyerere alisisitiza teknolojia rahisi na tiba asili zikijumuishwa na tiba za kisasa hususani katika huduma za msingi vijijini na akaweka msingi wa viwanda vya dawa kama Keko Pharmaceutical kilichopo Dar es Salaam ili kujitosheleza mahitaji ya dawa.
“Kwa ujumla, Mwalimu Nyerere aliona teknolojia kama chombo cha ukombozi wa kiuchumi kwa kusaidia kilimo, viwanda, elimu, afya na miundombinu. “Changamoto kubwa ilikuwa ukosefu wa mtaji na utaalamu, jambo lililosababisha baadhi ya miradi kutofanikishwa kwa kiwango alichotarajia,” anasema.
Dk Safari anasema kadri miaka inavyoenda ndivyo teknolojia inavyozidi kubadilika kadiri ya mahitaji ya wakati huo.
“Kwa sasa teknolojia inayotumiwa si inayozalishwa nchini, bali ni kutoka nchi nyingine lakini wakati wa uongozi wake Nyerere, alijitahidi kutengeneza teknolojia ya kwetu na aliamini inawezekana na jitihada zake kubwa ilikuwa ni Tanzania kuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zake yenyewe,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Safari, Nyerere alianzisha teknolojia iliyosifiwa na kuigwa ya uchimbaji udongo na kutambua madini ya chuma na kuyayeyusha kutengeneza chuma katika mikoa ya Tabora, Tanga, Moshi na baadaye ilitumiwa nje ya nchi.
Anasema Nyerere aliamini katika mgawanyo wa kazi za kimkoa kwamba kila mkoa utambulike na bidhaa au kitu
kitakachofanya kukuza biashara na nchi hususani kilimo. “Alijenga viwanda kwa kuzingatia malighafi zinazozalishwa eneo husika. Kwa mfano, Iringa aliona kuna miti mingi sana ndiyo maana akaweka kiwanda cha karatasi kinaitwa Mgololo,” anasema.
Katika muktadha huo wa kujitegemea, Baba wa Taifa (Nyerere) aliweka bayana kuwa kilimo pekee hakiwezi kufanikiwa bila kwenda sambamba na maendeleo ya viwanda na hivyo, kufanya kilimo kuwa cha kimkakati.
Profesa wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Abeli Kinyondo anasema Mwalimu Nyerere aliamini ili Tanzania iendelee lazima iwe na viwanda vya kutosha hasa viwanda vya umma kwani uchumi wa viwanda huliepusha taifa kutoka katika hali ya kuwa tegemezi.
Anasema viwanda hivyo vilijengwa kuimarisha uchumi kwa kutumia malighafi kutoka kwa wakulima wa ndani na kutengeneza bidhaa kabla ya kuuza katika soko la ndani na la nje ya nchi. Aidha, kulikuwa na viwanda vya kutengeneza bidhaa za viwandani, viwanda vya kuchakata kahawa vya Moshi na Bukoba, Kiwanda cha Sigara kilichopo Dar es Salaam na vingine vingi.
Anasema fikra za Nyerere zilikuwa sahihi kwani hakuangalia mnyororo wa thamani katika sehemu moja pekee, bali pia alioanisha kilimo na maendeleo ya viwanda huku akiweka bayana uhitaji wa kuwa na viwanda ili kuongeza thamani ya kilimo.
Profesa Kinyondo anasema Nyerere alisisitiza kuwa, ili taifa liendelee kwa namna mbalimbali ikiwamo ya kiuchumi, linahitaji ardhi, watu, siasa safi na uongozi bora na kwamba, ardhi ilitumika katika utawala wa Nyerere kuendeleza sekta ya kilimo ili kukuza uchumi kwa maendeleo ya kudumu.
Mchumi katika Taasisi ya Utafiti katika Kupunguza Umaskini (REPOA), Dk Donald Mmari anasema Nyerere alikuwa alilenga kuhakikisha Tanzania inajitegemea kiuchumi kwa kuzalisha bidhaa inazozitumia lakini zenye ubora wa kuuzika nje ya nchi.
Anasema Mwalimu Nyerere alisaidia uwekezaji na uzalishaji wa ndani kuhakikisha bidhaa zinazalishwa kwa
ubora na kulinda soko la wazalishaji wa ndani.
“Kwenye miaka ya 1973 moja ya hotuba zake aliwahi kusema uhuru tulioupata si mwisho wa safari, ni mwanzo wa kazi kubwa ya kujenga taifa huru. Tuliposema ‘Uhuru na Kazi’, tulimaanisha kwamba hatuwezi kujenga Tanzania mpya bila maarifa na teknolojia,” anasema.
Katika hotuba ya Azimio la Arusha mwaka 1967, Baba wa Taifa anasema teknolojia ni sehemu ya elimu. Anasema: “Maendeleo hayaji kwa miujiza, maendeleo huletwa na watu na watu hujengwa kwa elimu, bila teknolojia tutabaki wakulima wa jembe la mkono milele lakini tukitumia sayansi na uvumbuzi, tutaongeza uzalishaji na kuinua maisha ya wananchi.”
Katika hotuba yake kuhusu kilimo mwaka 1973, Nyerere anasema nchi inapaswa kubadili na kuboresha kilimo ili kiwasukume na kusukuma nchi. “Lakini isipokuwa kilimo hiki cha jembe la mkono, cha kutegemea mvua, hakina
mbolea, hakina dawa, hakina maarifa unalima halafu unapanda hovyo hovyo hakina tija,” anasema.
Anaongeza: “Kwa hiyo, teknolojia tunayohitaji si ya kifahari tu, tunataka teknolojia inayoweza kutumika vijijini ili kuwe na pampu za maji, zana bora za kilimo, umeme wa vijijini na njia rahisi za kusindika chakula.”
Nyerere anasema: “Teknolojia ni chombo na lengo letu ni uchumi wa kujitegemea na maisha bora kwa kila Mtanzania… Teknolojia itakuwa msaada wetu tu ikiwa itawekwa mikononi mwa wananchi na ikaendeshwa kwa manufaa ya wengi, si kwa faida ya wachache.”
Anaongeza: “Tuendelee kushirikiana, tujenge viwanda vyetu, tufundishe vijana wetu na tutumie sayansi na teknolojia kuinua Tanzania. Uhuru ni kazi na kazi ya maendeleo yetu haiwezekani bila teknolojia.
Make money while staying at home and working online. I just received $23,783 for my work last month, and I was doing this part-time. This year, I plan to earn even more, and I believe you can also make extra cash from this job. To join right now, follow the details on this website.
Open This… http://Www.Work99.Site