Nyota inayokufa yaitabiria dunia miaka bilioni 5 ijayo

KWA mara ya kwanza wanasayansi wameona nyota inayokufa umbali wa kiasi cha miaka 12,000 ya mianga.
Kwa mujibu wa taarifa za sayansi, mazingira ya kifo hicho yanaonesha ni kwa namna gani dunia hii tunayoishi itakavyomalizika miaka bilioni 5 ijayo.
Wanaastronomia ambao wameshuhudia kwa mara ya kwanza nyota inayofanana na jua letu ikiteketeza sayari wakati wa kifo chake, inatoa mwanga kwa dunia itakavyomalizika.
Wakati huo miaka bilioni 4 ijayo wakati jua linakufa, litavimba na kuimeza dunia kutoa mwanga juu ya hatima itakayoipata dunia kama ilivyotokea kwa nyota hiyo.
Kwa kuchambua takwimu mbalimbali zinazohusu nyota katika hatua mbalimbali za kuumbwa kwake, kuishi kwake na kufa, wanaastromia (wanasayansi) wamebaini kwamba nyota yetu (jua) mwisho wa uhai wake huanza kuchojoa msingi wa nishati inayoiendesha, hydrogen, iliyopo kwenye chanzo chake kigumu.
Hali hiyo inasababisha kusinyaa kwa chanzo hicho na sehemu zake za nje kuanza kutanuka na kupoa. Katika kipindi hiki nyota huongezeka kipenyo chake hadi mara 1,000 na hivyo taratibu kumeza sayari zilizo karibu zinazoizunguka.
“Tunajua kwamba hilo litatokea kwa kila sayari yenye mzunguko mdogo kuliko dunia yetu, lakini awali hatukufikiria kirahisi lakini sasa kwa hili tuliloliona tunaona inawezekana,” alisema mtafiti kiongozi wa tukio hilo la kifo cha nyota, Kishalay De, mfizikia wa anga za juu kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts.
Katika taarifa yake iliyonakiliwa na Space.com imeelezwa wanasayansi walikuwa wanachambua nyota zinazokufa baada ya kitendo kutokea lakini kwa sasa wameona kitendo chenyewe na kuona nini kitatokea katika dunia baadaye.
“Kusema kweli, nimeshangazwa na sisi kuona hili kwa mara ya kwanza,” alisema De na kuongeza: “Kumezwa kwa sayari kumekuwa kunatabirika katika uelewa wetu wa nyota, lakini tulikuwa na shida ya kufahamu mzunguko wake kwa uhakika. Hivyo kuona tukio hilo la nadra kwa mara ya kwanza tumesisimka sana.”
De na wenzake waliweza kupata taarifa hiyo baada ya kukagua mlipuko wa mionzi iliyopewa jina la ZTF SLRN-2020, tukio lililotokea mwaka 2020 kwenye diski ya Milky Way takribani miaka 12,000 ya mwanga, karibu na kundinyota la Aquila. Wakati wa tukio, nyota iliangaza kwa ukali wa zaidi ya mara 100 kwa wiki nzima.
“Kazi ilianza mwaka 2020 wakati sikuwa nikitafuta aina hii ya tukio,” De alisema na kuongeza: “Nilikuwa nikitafuta mlipuko wa kawaida inayoitwa novae.” Novas ni milipuko ya nyota ambayo hutoka wakati nyota inayokufa inapotema nishati yake kwenye sayari inayoambatana nayo.
Ugunduzi huo ulipatikana wakati wa uchambuzi wa takwimu zilizokusanywa na Zwicky Transient Facility, Kituo cha uangalizi wa anga cha Palomar kilichopo taasisi ya teknolojia ya California. Kituo hicho cha Zwicky Transient Facility huangaza anga kuangalia nyota ambazo hubadilika ghafla katika mnururisho wake, inayoweza kuashiria tukio la novas.
Ili ajifunze zaidi tukio hilo la ZTF SLRN-2020, De akachambua mwanga uliotokana na mlipuko huo ndipo alipobaini kuwa tukio hilo halifanani na nova kwa kuwa imezungukwa na gesi iliyopoa badala ya moto.
Kwa kawaida gesi iliyopoa inatokana na kuungana kwa nyota mbili.
De alifuatilia tukio hilo na takwimu zilizochukuliwa na Keck Observatory huko Hawaii alifanikiwa kuona molikuli ambazo zinaweza kupatikana baridi kali.
Kwa kawaida gesi baridi inaweza kuganda na kuunda vumbi baada ya muda.
Takribani mwaka mmoja baada ya ugunduzi huo wa awali, De na wenzake walichanganua data kutoka katika nyota hiyo kwa kutumia kamera ya infrared ya Palomar Observatory. Data ya infrared inaweza kuonesha uwepo wa mata ambayo ni baridi kinyume na mawimbi angavu ya mwanga yanayoonekana ambayo mara nyingi huambatana na matukio ya novas na mengine yenye nguvu.
Wanasayansi waligundua mlipuko mfupi wa mwanga ulioonekana kutoka katika nyota hiyo uliambatana na mwanga wa infrared ambao ulififia polepole katika kipindi cha miezi sita. Na kuthibitisha shaka ya De kwamba tukio hilo limetengeneza vumbi jingi.
Mchanganuo wa mwisho uliojibu maswali mengi ya kisayansi kuhusu tukio hilo ulipatikana katika takwimu zilizokusanywa na darubini ya anga ya infrared ya Nasa, Neowise.
Takwimu zilionesha kwamba mlipuko huo ulikuwa na nguvu ndogo kuliko kawaida ya nyota mbili kuungana kama ilivyoonekana hapo awali.
Kutokana na hesabu hizo ndipo walipobaini mlipuko huo haukuwa wa nyota zinazoungana bali sayari iliyovutwa katika nyota yake.
Kulingana na asili ya mlipuko huo, wanaastronomia walikadiria tukio hilo lilichojoa hewa haidrojeni sawa na takribani mara 33 ya uzito wa dunia, na vilevile vumbi lilikuwa ni 0.33 ya dunia. Kutokana na takwimu hizo wanadhani nyota hiyo ilikuwa takribani mara 0.8 hadi 1.5 ya uzito wa jua na sayari iliyochukuliwa ilikuwa karibu mara 1 hadi 10 ya uzito wa Jupita.
Kutokana na mazingira hayo dunia inatarajiwa kukutana na hali kama hiyo wakati jua litakapokuwa linavimba kuishia kiasi cha miaka takribani bilioni 5 ijayo.
“Iwapo ningekuwa nimekaa kwenye sayari umbali wa miaka 10,000 ya mwanga, kimsingi ningeona mwanga kutoka kwa mfumo wa jua japo utakuwa upo chini kidogo ikilinganishwa na huu tuliouona kwa sababu dunia ni ndogo kidogo kuliko sayari kama Jupita, ambayo tunaamini ndio iliyohusika katika tukio hili la kufa kwa nyota na hapa ndipo tunaona umuhimu wa ugunduzi huu katika mtazamo wa kibinadamu,” alisema De.
Ingawa kuna majibu ya mwisho wa dunia, lakini bado kuna maswali mengi wanasayansi wanajiuliza na jinsi wanavyochambua data watajua.
De anasema maswali haya yote kuhusu nini hasa kinaendelea kutokea katika mparaganyiko huo yatakuwa wazi wanapozidi kupata data zaidi juu ya tukio hilo.
Sasa kwa kuwa wanasayansi wanajua uwezekano wa kumezwa kwa sayari unavyoonekana kuendelea kufuatilia kunatoa jibu hali halisi ilivyo na hasa nadharia za sayari zenyewe zinavyoathiri nyota zao.
Makala haya yameandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya utafiti anga za juu.