MWANGA: NYUMBA zaidi ya 30 zimeathirika katika maporomoko ya udongo uliochanganyika na mawe yanayasababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika kata ya Kilomeni,wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya baadhi ya kaya zimelazimika kuomba hifadhi kwa ndugu wakihofia maafa zaidi kutokea.
Mbali na nyumba kuathiriwa pia miundombinu ya umeme na barabara imeathirika hali iliyopelekea kukosekana kwa mawasiliano kati ya kata ya Kilomeni na maeneo mengine kuwa ni changamoto kutokana na barabara kujaa vifusi .
Diwani wa kata ya Kilomeni Mohamed Mgallah akizungumza anasema tukio hilo limeathiri mashamba ya Mihogo, Mahindi na Migomba baada ya kuchukuliwa na maji na kwamba kwa sasa hakuna mashamba tena.
“Ni tukio ambalo si la kawaida lilitokea Januari 4 kuamkia Januari 05 mwaka huu ,kumenyesha mvua kubwa katika kata ya Kilomeni ambayo imesababisha maporomoko makubwa na kupelekea nyumba 33 kubomoka” amesema diwani Mgallah.
“Miundombinu ya barabara imeharibika sana,kwani barabara zimekatika na kumetokea vifusi vingi na vikubwa ambavyo vimefanya gari na pikipiki kushindwa kupita,……pamoja na hilo mawasiliano kati ya Kilomeni na sehemu nyingine bado ni changamoto kwasababu barabara ni mbaya sana.” Aliongeza Diwani Mgallah .