WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amewasimamisha kazi Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilombero (OCD) , Shedrack Kigobanya pamoja na Mkuu wa upelekezi wa wilaya hiyo (OC CID), Daud Mshana kutokana na kushindwa kwao kusimamia majukumu ya kazi zao na kusababisha wananchi kupata matatizo mengi.
Masauni ameziagiza mamkala zinazohusika kuwachunguza maofisa hao wa Polis,i ili kubaini madhira waliofanyiwa wananchi juu ya madai ya kunyanyaswa na askari yatakayowezesha kuchukua hatua stahiki pale yatakapothibitishwa.
Waziri Masauni alichukua hatua hiyo Februari 20,2023 baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofayika eneo la Stendi ya zamani ya mabasi mjini Ifakara, wilayani Kilombero.
“ Mliyozungumza hapa kwenye mkutano huu wa hadhara nimeyasikia na mliyozungumza kwa asilimia kubwa yana ukweli ndani yake na tayari serikali imeanza kuchukua hatua,” alisema Waziri Masauni.
Waziri Masauni amesema serikali kamwe haitakubali kuona mwananchi yeyote anaonewa na raia mwezake, au na mtu aliyepewa mamkala katika serikali pamoja na utumishi wa umma.
Waziri Masauni alisema Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Kilombero ameshindwa kufanya kazi yake vizuri ya kusimamia askari wake katika wilaya hiyo na kusababisha kujitokeza kwa mambo mengi.
“ Tunamsimamisha na tunamchunguza, sio yeye pekee yeke hata OC CID naye ataondolewa katika wilaya hii ya Kilombero, tunawaleteeni safu mpya ya viongozi wa jeshi la Polisi watakaokuja kufanya kazi ya wananchi,” alisema Masauni.