KITUO cha kisasa cha utafiti, uvumbuzi, ubunifu na ukarimu kinatarajiwa kujengwa eneo la Bungo Kibaha, mkoani Pwani.
Ujenzi wa kituo hicho ni kwa ajili ya kutoa wahitimu na watafiti ambao watakuwa na uwezo mkubwa wa kubuni, kuibua na kuanzisha ajira nyingi kwa Watanzania, ili kuchochea kukuza uchumi wa Tanzania.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ( OUT), anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu chuoni hapo, Profesa Deus Ngaruko amesema hayo alipotembelea Maonesho ya Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), yanayoendelea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Profesa Ngaruko amesema ujenzi huo unatarajiwa kuanza Julai mwaka huu katika eneo la ekari 105 huko mkoani Pwani.

Amesema ujenzi huo unatokana na Mradi wa Mageuzi ya Uchumi kupitia Elimu ya Juu (HEET) unaofadhiliwa na serikali, hivyo mpaka sasa maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho yanaendelea vizuri.
” Katika kituo hicho kutajengwa mashamba darasa ya mazao ya kilimo na mifugo, mabwawa ya kufuga samaki, mabwawa ya kusafisha majitaka, machinjio ya kisasa, ufugaji wa nyuki, maabara za sayansi, maabara za utalii na ukarimu, hosteli, nyumba za watalii pamoja na zoo ya wanyama,” amesema.
Kwa mujibu wa Profesa Ngaruko wafanyakazi katika uwekezaji huo mkubwa watakuwa ni wanafunzi wa chuoni hapo wanaosoma programu za astashahada, stashahada, shahada, shahada za umahiri na uzamivu.

“Sehemu kubwa ya vitu vitakavyotumika ndani ya kituo hicho ikiwemo chakula na mahitaji mengine yote yanatarajiwa kuzalishwa hapo hapo.
“Hakika, hii ndivyo namna OUT inavyotaka kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya serikali ya kuhakikisha vyuo vikuu vinaandaa mitaala na mazingira ya kuzalisha wahitimu ambao watakuwa na uwezo wa kujitegemea kwa kuanzisha ajira kwao wenyewe na kwa wanajamii wote wa Tanzania,” amesema.
Profesa Ngaruko ni mratibu Mkuu wa mradi huo wa HEET kwa chuo.