Papa asikitishwa na vita Gaza, asema silaha hazileti amani

VATICAN CITY, Vatican: KIONGOZI wa Kanisa
Katoliki Duniani, Papa Francis amesikitishwa na hali ya vita inayoikabili dunia kwa sasa na kuitaka jumuiya ya kimataifa kufanya kila liwezekanalo kusitisha vita Gaza na Ukraine.

Papa Francis amesema hayo jana katika Jiji la Vatican wakati alipokuwa akitoa ujumbe wake wa Pasaka kwa waumini wa Kanisa hilo duniani na kuongeza kuwa amani hailetwi kwa silaha.

Bila kuficha, Papa Francis alitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Hamas huko Gaza pamoja na kuachiliwa kwa mateka wote wanaoshikiliwa na Kundi la Hamas.

Papa Francis aliongoza sherehe ya Pasaka huko Vatican ikiwa ni siku muhimu zaidi katika kalenda ya Kikristo ambapo Wakristo wote duniani hukumbuka kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo.

Misa hiyo iliyohudhuriwa na maelfu ya waumini ilifanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro.

Katika hotuba yake ya kitamaduni inayorushwa kote duniani, Papa Francis alilaani vita akivitaja kuwa ni upuuzi, akigusia pia mizozo nchini Ukraine, Gaza,
Sudan, Myanmar na kwingineko.

“Tusiruhusu upepo wa vita uvume Ulaya na eneo la Mediterania. Tusikubali mantiki ya
matumizi ya silaha na kujihami tena na silaha,” ameongeza.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani pia amewahimiza viongozi wa dunia wafanye juhudi kupambana na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu na
kuwaokoa wahanga.

Habari Zifananazo

Back to top button