PAPA FRANCIS; Taa ya unyenyekevu, amani ‘iliyozimika’

PAPA Francis ni Papa pekee (Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani), aliyeshiriki kumchagua papa (mtangulizi wake) Papa Benedicto XVI mwaka 2005 akiwa Kardinali kisha akamzika mwaka 2022 yeye sasa akiwa Papa hivyo, kuwa Papa wa kwanza kwa zaidi ya karne moja kumzika mtangulizi wake.

Machi 13, 2013 alijitokeza kwenye roshani katika Viwanja vya Mtakatifu Petro maarufu, St Peter’s Square, akiwa amevalia mavazi meupe tu.

Alipewa jina jipya lililomtukuza Mtakatifu Francis wa Assisi aliyekuwa mhubiri wa Karne ya 13 na mpenda wanyama.

Huyu, ndiye papa wa kwanza kutumia jina la Francis; Papa wa ‘sauti ya unyenyekevu, heshima na ukarimu’ na  Mjesuti wa kwanza kuchaguliwa kwenye kiti cha enzi cha Mtakatifu Petro.

Mtangulizi wake, Papa Benedicto XVI (Joseph Ratzinger) naye aliweka historia katika kiti cha upapa kwa kustaafu kwa hiari na kuifanya Bustani ya Vatican kuwa mwenyeji wa mapapa wawili.

Ndiye huyo, Papa Francis ambaye sasa ‘amekwenda’ amekufa akiwa amewahudumia waumini wake katika Kanisa Katoliki duniani wapatao bilioni 1.4 kwa takribani miaka 12 sasa; tangu mwaka 2013.

Kitendo chake cha mwisho kama Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani kilikuwa kuonekana Jumapili ya Pasaka kwenye roshani ya St Peter’s Square, akiwapungia mkono maelfu ya waumini baada ya wiki kadhaa hospitalini akiwa na nimonia mara mbili.

Si tu Wakatoliki wanaomlilia, bali watu wa mataifa, dini na kada mbalimbali wakiwamo waamuni, viongozi wa kanisa hilo katika mataifa mbalimbali na hata viongozi wa dini nyingine.

Hii ni kwa kuwa Papa Francis (Jorge Mario Bergoglio), alikuwa sauti ya heshima na ukarimu iliyojaa upendo, unyenyekevu usiofichika na hamu ya haki na amani kwa kila mtu. ‘Amekwenda’.

Papa Francis, Kiongozi Mkuu wa 266 wa Kanisa katoliki Duniani, ameondoka duniani akiwa ameacha alama nyingi zisizofutika za kuwa mchungaji mnyenyekevu aliyependa ushirika na watu wa hali ya chini na ulinzi wa tunu ya amani.

Ameondoka katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka, Jumatatu ya Pasaka Aprili 21, 2025 akiwa na umri wa miaka 88 huku akiwa kiongozi wa kimataifa asiyekuwa na mipaka ya upendo, haki na unyenyekevu usio na mipaka.

Mapapa wanne waliomtangulia na majina yao halisi waliyotumia kabla ya majina ya upapa na vipindi vya uongozi wao katika mabano ni Papa Paul VI (Giovanni Battista Enrica Antonio Maria Montini) -(1963 – 1978),  Papa John Paul l (Albino Lucian – 1978- 1978), Papa John Paul ll (Karol Jozef Wojtyla- 1978 – 2005) na Papa Benedict XVI (Joseph Ratzinger- 2005- 2013).

Papa Benedict wa 16

Vatican; makao makuu ya Kanisa Katoliki Duniani sasa hayana Papa. Yanaongozwa na Camerlengo.

Camerlengo ndiye Kaimu Mkuu wa Vatican hadi Papa mwingine anapochaguliwa.

Ndiye huandaa mchakato wa uchaguzi wa papa unaohusisha makardinali wote wenye umri usiozidi miaka 80 hao ndio huwa na haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa papa.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Padri Charles Kitima, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Mwadhama Protas Kardinali Rugambwa ni miongoni mwa makardinali watakaoshiriki kuchagua au kuchaguliwa kuwa Papa wa 267.

“Sisi tuna bahati tumepata kardinali mpya mwaka juzi (Protase Rugambwa) … Watanzania tuna mshiriki atakaenda kupiga kura ama kupigiwa kura,” anasema Padri Kitima.

Kwa niaba ya Watanzania, Rais Samia Suluhu Hassan anasema, “Nimesikitishwa na taarifa ya kifo cha Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis. Katika kipindi chote cha miaka 12 akiwa kiongozi wa kanisa hilo, ameishi kama mwalimu aliyefundisha na kuhimiza ustawi na maendeleo ya watu, pamoja na kudumisha amani.”

Februari 2024, Rais Samia alizungumza na kiongozi huyo wakati wa ziara yake ya kihistoria mjini Vatican akiwa Rais wa kwanza kutoka Tanzania kutembelea Makao Makuu ya Kanisa Katoliki baada ya zaidi ya miaka 15.

Mazungumzo yao yalilenga mchango wa Kanisa Katoliki Tanzania, hususani katika sekta za elimu, afya na maendeleo ya kijamii.

Viongozi wengi duniani wametuma salamu za rambirambi kuhusu kifo cha Papa Francis huku Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas akisema anamkumbuka Papa kama ‘Rafiki wa Kweli’ wa watu wa Palestina.

Kwa mujibu wa taarifa na vyanzo mbalimbali, kifo cha Papa Francis kilithibitishwa Jumatatu ya Pasaka kupitia vyombo vya habari vya kimataifa zikibainisha kuwa, alifariki dunia katika makazi yake ya Casa Santa Marta, Vatican, saa 1:35 asubuhi kwa saa za Roma, baada ya kuugua nimonia kali.

Taarifa hizo zilitolewa na Mwadhama Kelvin Kardinali Farrell aliposema, “Askofu wa Roma, Francis, amerejea katika Nyumba ya Baba.”

Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Diego Ravell wa Vatican, Papa Francis aliomba mazishi yake yawe ya kawaida.

 

Kabla ya mauti

Kabla ya kufikwa na mauti taarifa kutoka Vatican zinasema, Papa alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya mfumo wa upumuaji, hali iliyosababisha kufuta baadhi ya ziara zake zikiwemo za Umoja wa Falme za Kiarabu mwaka 2023.

Alilazwa katika Hospitali ya Agostino Gemelli, Februari 14, 2025 na hali yake ilizidi kuwa mbaya Februari 18, kabla ya kurejea nyumbani baada ya siku 38 hospitalini.

Awali Julai, 2021 vyombo vya habari vinasema mtandaoni kuwa, alikaa hospitalini kwa siku 10 kufuatia upasuaji wa utumbo mwembamba.

Machi 2023, alilazwa hospitalini kwa siku tatu. Miezi michache baadaye, Juni 2023, alirudi hospitalini kufanyiwa upasuaji wa utumbo.

Tangu 2022 mara nyingi alitumia kiti cha magurudumu, kitembezi au fimbo kutokana na majeraha ya goti kutokana na kuanguka mara nyingi.

Akiwa mzee pia alipatwa na maumivu kwenye goti lake la kulia, ambayo aliyataja kuwa ni ‘unyonge wa mwili’.

 

 

Maisha ya Papa Francis

Alizaliwa Desemba 17, 1936 mjini Buenos Aires, Argentina. Alichaguliwa kuwa Papa wa 266 Machi 2013, akiwa Papa wa kwanza kutoka Bara la Amerika, Papa wa kwanza kutoka Shirika la Kijesuiti na Papa wa kwanza kutoka nje ya Ulaya kwa zaidi ya miaka 1,000.

Katika uongozi wake amejulikana kwa unyenyekevu, kujitoa kwa jamii, kuwatumikia masikini, kulinda mazingira na kuhimiza upendo na amani duniani.

Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Maggid Mjengwa amenukuliwa na HabariLEO Afrika Mashariki toleo la jana akisema Papa Francis atakumbukwa kwa msimamo wake wa kupigania amani duniani, kukemea mauaji ya wanawake na watoto wa Palestina katika Vita ya Gaza pamoja na mageuzi makubwa ndani ya Kanisa Katoliki.

Kwa mujibu wa Mjengwa, kiongozi huyo ni miongoni mwa viongozi wachache wa dini waliokemea vikali ukiukwaji wa haki za binadamu na alijitokeza kuwapatanisha viongozi wa Sudan Kusini, hatua iliyosaidia kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Unyenyekevu na upatanishi

Katika ziara nchini Sudan Kusini Aprili, 2019  Papa Francis alifanya tendo kubwa la unyenyekevu  kwa kupiga magoti na kubusu miguu ya viongozi hasimu wa Sudan Kusini (Rais Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar) kuwahamasisha kuendeleza mchakato wa amani.

Januari, 2015 alipozuru Ufilipino, nchi yenye Wakatoliki wengi zaidi barani Asia, aliendesha ibada ya misa iliyohudhuriwa na waumini milioni sita idadi inayoonekana kuwa ya kwanza katika historia ya upapa.

Septemba 24, 2015 Papa Francis aliweka historia ya kuwa papa wa kwanza kuhutubia Bunge la Marekani huku akitoa mwito kwa bunge hilo na wananchi kuweka pembeni tofauti zao na kurudisha roho ya urafiki na umoja, ukarimu na kushirikiana.

Mwaka 2014 aliwakutanisha Rais wa Israel, Shimon Peres na mwenzake wa Palestina, Mahmoud Abbas kuombea amani.

Francis alifanya kazi na Waanglikana, Walutheri na Wamethodisti na kuwashawishi marais wa Israeli na Palestina kuungana naye kuombea amani.

Baada ya mashambulizi ya wapiganaji wa Kiislamu, alisema si sawa kuutambulisha Uislamu na vurugu. Akasema, “Ikiwa nitazungumzia ghasia za Kiislamu, basi lazima nizungumzie vurugu za Wakatoliki pia.”

Muda mfupi baada ya kuwa Papa mwaka 2013, alishiriki maandamano ya kupinga utoaji mimba huko Roma huku akitoa wito wa haki za watoto ambao hawajazaliwa; tangu kutungwa kwa mimba”.

Alipinga kuwekwa wakfu kwa wanawake, akitangaza kwamba Papa Yohane Paulo wa Pili alikuwa amepuuza uwezekano huo.

Mwaka wa 2015 akiwa Ufilipino, alisema uzazi wa mpango unahusisha ‘kuharibiwa kwa familia kwa kunyimwa watoto.’

Vyanzo mbalimbali vinamtaja Papa Francis kama kiongozi wa dini aliyeishi maisha ya kawaida, tofauti na mawazo ya watu wengi kuhusu viongozi wa juu wa dini.

Chapisho moja la shirika la Habari la Uingereza (BBC) mtandaoni linasema tangu kuchaguliwa kwake, aliazimia kupendelea unyenyekevu kuliko fahari na alionesha kuwa atafanya mambo tofauti.

Papa Francis alipokea makardinali wake isivyo rasmi kwa kusimama badala ya kuketi kwenye kiti cha upapa.

Shirika la habari la Catholic News Service (CNS) limewahi kunukuliwa likimripoti papa akitaja baadhi ya kazi alizowahi kufanya kuwa ni pamoja na kuwa mwalimu wa Saikolojia pamoja na Fasihi na kwamba, amewahi pia kuwa mfanyakazi wa maabara.

Kwamba, Papa alibainisha hayo alipotembelea Kanisa la San Cirillo Alessandrino huko Rome, Italia Desemba 5, 2013 na kuongeza kuwa, pia Papa Francis aliwahi kuwa baunsa wa Klabu ya Usiku ya ya Buenos Aires, akiwa mwanafunzi.

Kutokana na msiba huo wa kidunia, TEC limetangaza siku tisa mfululuzo za maombolezo za kiongozi huyo wa kiroho.

Katika mkutano na wandishi wa habari kuhusu kifo hicho Dar es salaam juzi, Dk Kitima (Katibu Mkuu TEC) anazungumzia maisha ya Papa Francis, akisema alikuwa ni kiongozi mwenye huruma aliyependa kuona watu wakitoka katika dimbwi la umasikini kwa kuwezeshwa kupitia njia mbalimbali ili wasirudi katika umasikini.

“Alipochaguliwa alitoa mfano, alisema jamani kama kuna mtu ana jozi nne za viatu jozi moja si ya kwako unapaswa kuwa na jozi tatu hiyo jozi moja mpe mwingine ambaye hana,” anasema Padri Kitima.

Anafafanua kuwa, kutakuwa na misa kila siku katika kipindi hicho cha maombolezo na haijafahamika atazikwa lini.

Anafahamisha kuwa, papa mpya atapatikana ndani ya siku 15 hadi 20 na atachaguliwa miongoni mwa makardinali wenye umri wa chini ya miaka 81 kutoka duniani kote watakaokutana na kumchagua papa mpya miongoni mwao.

Kuhusu papa ajae baada kifo cha Papa Francis, Padri Kitima anasema jambo hilo lipo mikononi mwa Mungu; ndio anafayefahamu ni kiongozi gani atafuata na atatokea wapi kutokana na uhitaji wa Kanisa duniani.

Kwa mujibu wa Padri Titus Napemba ambaye ni Mwanafunzi wa Mwasiano aliyeko Vatican, Papa Francis alipenda watu masikini akisema naye (papa) ni miongoni mwa masikini.

“Alipenda usawa haki na amani,” anasema katika mazungumzo na kituo cha televisheni cha UTV juzi usiku.

Padri Ngapemba anasema, “Hivi karibuni aliwekwanda kusali kwenye makaburi ya mapapa akiwa amevaa mavazi ya kawaida kabisa na watu wakabaki wameshangaa. Inawezekana alitaka kusema anajiandaa kwa kifo maana baada ya muda mfupi (siku si nyingi) amefariki dunia.

Kuteuliwa katika Kanisa

Mwaka 1992 aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Buenos Aires na baadaye mwaka 1998 Papa Yohane Paul II akamteua kuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires.

Mwaka 2001, Papa Yohane Paulo II alimteua kuwa kardinali.

Papa Francis aliteua zaidi ya makardinali 140 kutoka nchi zisizo za Ulaya na kumwacha mrithi wake Kanisa ambalo lina mtazamo wa kimataifa zaidi.

Alipania kuimarisha utume wa kihistoria wa Kanisa kwa kukata migogoro ya ndani akiwalenga masikini na kurudisha Kanisa kwa watu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button