DAR ES SALAAM: Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imeibuka kinara baada ya kutwaa tuzo ya mzalishaji bora wa pombe kali katika Tuzo za Rais kwa Wazalishaji Bora (PMAYA) 2024.
Tuzo za PMAYA, ambazo ni miongoni mwa heshima za juu kabisa kwa wazalishaji nchini Tanzania, zimeundwa kutambua na kuhamasisha ubora kwa wazalishaji katika sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, aliipongeza timu nzima ya SBL kwa juhudi zao na kusisitiza dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kuboresha ubora wa bidhaa zake huku ikichangia katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
“Tumeweka mkazo katika kuunda bidhaa zinazozingatia viwango vya ubora na uendelevu ili kukidhi na kuvuka viwango vya sekta, na kuweka kampuni katika nafasi ya pekee kama mdau muhimu katika sekta ya uzalishaji nchini Tanzania,” alisema.
Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango alimwakilisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan kama mgeni rasmi.
Dk Mpango alieleza kuwa Serikali imeimarisha miundombinu ya barabara na bandari ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa nje na ndani ya nchi, kwa lengo la kusaidia mafanikio ya sekta ya viwanda.
SOMA: Ripoti mpya ya SBL yaweka mkazo ushirikishwaji, ujumuishwaji
Aidha, aliwahimiza wazalishaji kuongeza juhudi katika uzalishaji na kuongeza bidhaa za katikati (intermediate goods) ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
SBL imeahidi kuendelea kuiunga mkono uchumi wa Tanzania kwa kuwekeza zaidi, hususan katika sekta ya kilimo.
Kwa sasa, zaidi ya asilimia 75 ya malighafi inayotumika katika uzalishaji wa bia zake inapatikana nchini, na hivyo kunufaisha moja kwa moja wakulima wa Kitanzania na kuimarisha mnyororo wa ugavi wa kilimo nchini.
Kwa kutilia mkazo ununuzi wa ndani, SBL inalenga sio tu kupunguza utegemezi wa uagizaji, bali pia kuwawezesha jamii za vijijini, kuunda ajira, na kuendeleza kilimo endelevu.
Uwekezaji huu unaendana na dhamira kuu ya SBL ya kusaidia viwanda vya ndani, kukuza uchumi, na kuchangia kujitosheleza kwa Tanzania katika rasilimali muhimu za uzalishaji.