Wahimizwa kufanya tafiti zenye tija

MWANZA: WATAFITI nchini wametakiwa kufanya tafiti zenye tija na kuhakikisha matokeo ya tafiti hizo yanawafikia wananchi ili kuchangia utatuzi wa changamoto za jamii na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Rai hiyo imetolewa leo Novemba 25, 2025 jijini Mwanza na Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Serikali, Benjamin Magai, katika uzinduzi Kongamano la Nne la Kimataifa la Usimamizi wa Biashara na Ukuaji wa Uchumi, linaloratibiwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).
Magai alisema kuna umuhimu mkubwa kwa watafiti kufanya tafiti zenye matokeo yanayoweza kutumiwa na watunga sera na wadau mbalimbali, ili kuwezesha maendeleo ya kijamii na kiuchumi kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia.
Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania(TIA), profesa William Pallangyo amesema kongamano hilo ambalo linaendelea jijini Mwanza, limewakutanisha watafiti, wataalumu, wadau wa biashara na uchumi kutoka ndani na nje ya nchi, ikiwa ni mwendelezo wa jitihada za TIA kuimarisha tafiti, mafunzo na ushauri wa kitaalam tangu kuanzishwa kwa makongamano hayo mwaka 2022.
Amesema dhima kuu ya kongamano la mwaka huu ni Uvumbuzi, Ubunifu na Biashara kwa Uchumi Endelevu. Amesema kuwa baada ya majadiliano ya tafiti, taasisi hiyo itatayarisha kitabu maalum chenye mapendekezo ya kitaalam kuhusu namna bora ya kukabiliana na changamoto zilizobainishwa.



