Polisi Mwanza yamshikilia Dk Nawanda

MWANZA – POLISI jijini Mwanza imemtia mbaroni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda kwa tuhuma za kumwingilia kimwili kinyume na maumbile mwanafunzi wa kike (jina linahifadhiwa) wa chuo kikuu kimoja kilichoko jijini Mwanza.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alisema jana kuwa Dk Nawanda alikamatwa jana jijini Mwanza saa 6:00 mchana na kuwekwa mahabusu katika kituo kikuu cha polisi cha mkoa.

Alisema Jeshi la Polisi limemkamata na kuendelea kumhoji Nawanda (46) ambaye pia ni mkazi wa Mtaa wa Nyaumata katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu.

Alisema tukio hilo la kumwingilia kimwili mwanafunzi ni la Juni 2, mwaka huu usiku katika eneo la Rock City Mall, Mtaa wa Ghana wilayani Ilemela.

Alisema sasa Jeshi la Polisilinaendelea kufanya mahojiano na mtuhumiwa yanayokwenda sambamba na kukamilisha uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikisha taasisi za uchunguzi wa kisayansi.

Alisema uchunguzi utakapokamilika, jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua nyingine muhimu za kisheria. “Mtuhumiwa huyo amekamatwa, anahojiwa kwa kuzishirikisha taasisi za kiuchunguzi zilizoko jijini Mwanza,” alisema.

Aliwataka wananchi kutojihusisha katika utoaji wa taarifa za matukio ya ukatili kwenye mitandao ya kijamii kwa namna ambayo inaendelea kumuumiza mwathirika wa tukio hilo la kikatili.

“Mwathirika anaendelea kuumia kisaikolojia kutokana na namna ambavyo watu wanavyoendelea kuripoti matukio hayo,” alisema na kuongeza utoaji wa taarifa za aina hiyo una misingi yake inayohifadhi utu wa mtu.

Kuhusu kuwapo kwa taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo ya mlalamikiwa kuachana na shauri hilo kwa madai kuwa anatumiwa kisiasa, kamanda alisema hakuna mahali popote ambapo polisi wanaruhusiwa kwa mujibu wa sheria kuruhusu majadiliano ya aina yoyote shauri nje ya mahakama.

“Kwa msingi upi, mlalamikaji katika makosa haya ya kijinsia ni Jamhuri na yule mtendewa ni shahidi tu, huo ndio msingi pekee ulio hapo,” alifafanua.

SOMA: 2023: Watu wanne walikufa kwa ajili kila siku 

Alisema taarifa za kufutwa kwa shauri na taarifa hiyo iliyotolewa kwenye mitandao ya kijamii si ambayo ilipokewa katika kituo cha polisi jijini Mwanza.

“Hiyo taarifa sio sehemu ya upelelezi wa jalada letu na sisi tunaiona, lakini mlalamikaji ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mtendewa anabakia kuwa shahidi,” aliongeza.

Kamanda Mutafungwa alifafanua kuwa makosa hayo ni tofauti na ya mtu kutukanwa au kupigwa kofi ambayo anaweza kufanya majadiliano. “Lakini sio kwa makosa yanayohusisha ukatili wa kijinsia na watoto,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button